Habari za Kitaifa

Juhudi za kutoa kadi ya ushahidi katika tumbo la mshukiwa zaingia siku ya pili

Na RICHARD MUNGUTI August 7th, 2024 2 min read

MATUMAINI ya Polisi kupata kadi ya kuhifadhi data iliyomezwa na mshukiwa katika kashfa ya kutengeneza hatimiliki feki za mashamba yamepigwa jeki na mahakama ilipoamuru Agosti 6, 2024 ombi lingine liwasilishwe kuamuru Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) itumie kila mbinu itoe kadi hiyo kutoka kwa utumbo wa Joel Kakuli Mwangangi.

Akitoa uamuzi katika kesi ambapo washukiwa sita wanapigwa darubini na polisi kwa kutengeneza hatimiliki feki za mashamba, hakimu mkuu Mahakama ya Milimani Bernard Ochoi aliagiza polisi wawasilishe ombi lingine ambapo afisa mkuu KNH ataagizwa ampime Joel kubaini ikiwa kadi hiyo ingali ndani ya utumbo au la.

Bw Ochoi alisema polisi wanaamini kadi hiyo iliyo na ushahidi wote katika kashfa hiyo ya hatimiliki feki wanayochunguza lazima “itolewe kwa vyovyote vile.”

Kiongozi wa mashtaka James Gachoka alimweleza hakimu kesi hiyo itasambaratika ikiwa ushahidi huo wa kadi ya kuhifadhi data haupo.

“Naomba mahakama iwape polisi fursa nyingine ya kuwasilisha ombi lingine wakiomba maagizo yatolewe kwa afisa mkuu KNH afanye kila juhudi kupata kadi hiyo. Ushahidi wa kadi ndio uti wa kesi hii. Bila ushahidi huo kesi hii itaporomoka na washukiwa kuachiliwa huru,” Bw Gachoka alimweleza hakimu.

Mnamo Agosti 5, 2024 Koplo Nicholas Osuri Otieno aliwasilisha ombi aruhusiwe kumpeleka Joel KNH akatolewe kadi aliyomeza kwenye utumbo wake.

Koplo Otieno alisema mbinu polisi walizojua “za kuitoa kadi hiyo ndani ya utumbo wa Joel Kakula Mwangangi hazikufua dafu.”

Akafichua,“Tulimpeleka Joel kituo cha polisi cha uwanja wa ndege wa kimataifa JKIA ambapo washukiwa wa mihandarati huzuiliwa na kupewa ugali na maziwa mala kutaga vidonge vya dawa za kulevya ambazo huwa wamezimeza lakini hatukufaulu kupata kadi hiyo.”

Koplo Otieno alisema baada ya Joel kulishwa ugali na maziwa mala alienda choo lakini haikuwa na kadi hiyo.

Choo hicho kilichoko JKIA ni maalum kwa vile mmoja akienda haja kubwa huloweshwa maji kisha ushahidi unaosakwa hutolewa na kuoshwa kwa maji safi na kufikishwa kortini kama ekzibiti.

“Sasa kilichosalia ni Joel apelekwe KNH kupimwa kwa kupigwa X-ray ama Scan ndipo kadi ionekane ilikokwama kwenye utumbo.”

Koplo Otieno alisema “lazima kadi hiyo ipatikane”

Joel anadaiwa alimeza kadi hiyo alipofumaniwa na polisi katika jengo moja eneo la Ngara anakodaiwa hutengeneza hati feki za kumiliki mashamba.

Joel alikamatwa pamoja na Benedict Mwangangi Ngala, Vincent Boaz Owang, Titus Wambua Kithuku, Sylvester Mwanzia Mwanthi na Eric Omondi Ojwang.

Sita hao, hakimu alifahamishwa walikamatwa wakiwa na hatimiliki feki za mashamba 399 na barua za ugavi wa mashamba za eneo la Mweiga kaunti ya Nyeri.

Mahakama ilieleza kutolewa kwa kadi hiyo kutakuwa na manufaa kwa afya kwa Joel sawia na kufanikisha uchunguzi.

Mahakama ilielezwa Joel alimeza kadi hiyo kuharibu ushahidi wa utengenezaji hati feki ulioko ndani yake.

Ushahidi kwenye kadi hiyo niwa kuhusu hati feki 399 walizokuwa wanachapisha.

Polisi wanataka kubaini majina kwenye hati hizo.

Pia uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu uhakiki wa mabarua ya wakuu wa idara ya ardhi waliyokutwa nayo.

Bw Gachoka alimsihi hakimu aruhusu Mawakili wakiongozwa na Felix Kiprono waliomba washukiwa waachiliwe kwa dhamana wakisema “ombi la upande wa mashtaka halina mashiko kisheria.”

Mahakama ilielezwa washukiwa walitiwa nguvuni na mamia ya hatimiliki mashamba na mabarua ya idara ya usorovea, hatimiliki feki za mashamba, mawasiliano kutoka kwa msajili mkuu wa hatimiliki na mabarua kutoka kwa wakurugenzi wa idara ugavi wa mashamba.

Hakimu aliamuru washukiwa walipe dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu kwa vile mashine na hati miliki feki za mashamba ambazo zitachunguzwa tayari zimechukuliwa na polisi.

Kuhusu Joel, Bw Ochoi alisema “polisi wawasilishe ombi lingine. Hata naye yuko huru kulipa uchunguzi uendelee akiwa nje.”

Bw Ochoi aliwaagiza washukiwa hao sita wasivuruge uchunguzi.

Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili.