Habari za Kitaifa

TSC yazindua marupurupu ya kuvutia walimu katika shule za walemavu

Na MARY WANGARI August 8th, 2024 2 min read

TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imeanzisha malipo ya marupurupu kwa walimu katika shule za watoto walemavu katika juhudi za kuwavutia na kuwadumisha katika taasisi hizo.

Haya yanajiri huku Shule za Watoto Walemavu zikikabiliwa na uhaba wa walimu 5,362, ikileleza Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utangamano na Nyadhifa Sawa.

Mkurugenzi wa TSC, Nancy Macharia, aliambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mandera Kaskazini, Adan Haji, kuwa vifaa maalum vinavyofahamika kama Nyenzo za Wasomaji vimeanzishwa kwa walimu walemavu ikiwemo vipofu, viziwi, bubu na wengineo.

“Malipo haya yatajumuishwa kwa marupurupu ya kawaida kisheria kama vile kwa wanaofanya kazi katika mazingira magumu, usafiri miongoni mwa mengine, kama njia moja ya kutambua changamoto za ziada zinazowakabili walimu,” alisema Bi Macharia, alipofika mbele ya Kamati hiyo Jumanne.

“Marupurupu ya Shule za Walemavu ni malipo mengine yaliyoanzishwa kwa walimu wenye ujuzi kuhusu elimu ya walemavu.”

Kuhusu uhaba wa walimu, Bi Macharia alisema TSC iliajiri na kuwatuma kazi jumla ya walimu 1,763 mwezi Mei.

Alisema kuwa kundi lingine la walimu 3,600 wataajiriwa mwezi ujao mwaka huu, Januari na Juni mwaka ujao.

“Kutokana na vikwazo vya bajeti, tume imebuni mchakato wa kuwaajiri kwa vitengo walimu katika shule za walemavu ili kutatua uhaba uliopo,” akasema Bi Macharia.

Kulingana naye, tume hiyo imeanza kutekeleza mfumo maalum kwa shule za elimu ya walemavu unaozingatia ukubwa wa darasa, aina na kiwango cha ulemavu, kwa wanafunzi wanaofunzwa na kila mwalimu.

Alisema hatua hiyo inadhamiriwa kuhakikisha walimu wanawashughulikia kikamilifu wanafunzi walemavu.

“Ukubwa wa darasa, kwa mfano, lenye wanafunzi walio na matatizo ya kiakili litakuwa na wanafunzi wanne. Darasa lenye wanafunzi wenye ulemavu wa kimwili litakuwa na wanafunzi 15,” akafafanua.

“Kadri idadi ya wanafunzi walemavu ilivyo ndogo kwa kila mwalimu, ndivyo utowaji huduma unavyozidi kuwa bora.”

Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Liza Chelule, aliyeongoza kikao hicho, alisema TSC ingali na kibarua cha kuboresha maslahi ya walimu katika shule za walemavu huku akipongeza hatua zilizopigwa.

Mwakilishi Mwanamke huyo wa Kaunti ya Nakuru alisema, “Kamati ilizuru shule za walemavu katika maeneo ya Pwani, Nyanza, Magharibi na Bonde la Ufa na kubaini kuwa shule na walimu wanafanya kazi katika mazingira duni.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Shinyalu, Fredrick Ikana alielezea wasiwasi wake kwa masaibu yanayowakumba walimu katika shule za walemavu yanawavunja moyo wenzao kusaka kazi katika taasisi hizo kwa hivyo kusababisha upungufu.