ODM ilitumia vitisho Oparanya akaidhinishwa na kamati ya uteuzi kuwa waziri
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kilitishia kukataa uteuzi wa maafisa wake katika serikali ya Rais William Ruto iwapo aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya hangeidhinishwa na Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu Uteuzi, Taifa Dijitali imeweza kufichua.
Kamati ilichukua saa nne kujadili suala la Oparanya, kikao ambacho inasemekana kilikumbwa na malumbano makali.
Bw Oparanya aliidhinishwa kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika.
Awali, kamati hiyo ilikuwa imekubaliana kuchukua chini ya dakika 30 kuidhinisha ripoti ambayo ilikuwa imetayarishwa na wafanyakazi wa bunge ikipendekeza kupitishwa kwa wote walioteuliwa.
Kamati ilirejea kwenye kikao cha faragha ambapo sekretarieti nzima ilitolewa nje na kuwaacha wanakamati wakijadili kuhusu nani wangekataa kuidhinisha.
Ingawa upande wa ODM wa kamati hiyo uliripotiwa kutokuwa na shaka na wote walioteuliwa, haukujua mipango ambayo upande wa Kenya Kwanza ulikuwa nayo.
Upande wa serikali ulikuwa na maoni kwamba Bi Stella Lang’at hakufanya vyema wakati wa mahojiano na kwa hivyo hakustahili kuidhinishwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi.
Akitoa taarifa kuhusu ripoti ya kamati Bungeni mara baada ya kuiwasilisha, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah alisema: “Kwa kuzingatia matokeo ya Kamati ya Uteuzi katika ripoti yake ya pili iliyowasilishwa, Bunge linaidhinisha walioteuliwa na kukataa uteuzi wa Bi Stella Lang’at.”
Upande wa Kenya Kwanza ulipendekeza kwamba uteuzi wa Bw Oparanya ukataliwe kwa sababu ya matatizo yake na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
EACC ilimwandikia karani wa Bunge la Kitaifa kupinga uteuzi wa Bw Oparanya, ikisema anachunguzwa kwa ufisadi, jambo ambalo amekanusha.
“Ni wakati huo ambapo Junet Mohammed alisimama na kusema kuwa kamati hiyo ijumuishe Bw Oparanya miongoni mwa waliopendekezwa kuidhinishwa au ODM iachane na nyadhifa za uwaziri ilizotengewa,” alisema mwanachama wa timu hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina. .
Bw Mohammed hakujibu maswali ya Taifa Dijitali kuhusu tukio hilo.
Kuidhinishwa na kamati inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kulipisha kuapishwa kwa walioteuliwa Alhamisi, Agosti 8, 2024.