Habari Mseto

Tumia uwaziri wako kuinua Magharibi, Aladwa aambia Oparanya

Na KEVIN CHERUIYOT August 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Makadara George Aladwa amemtaka Waziri mpya wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Wycliffe Oparanya kutumia wadhifa wake kusaidia wakazi wa eneo la Magharibi mwa Kenya.

Bw Aladwa alisema kuwa wakati umefika ambapo jamii ya Mulembe inastahili kunufaika na uwepo wa viongozi wao ndani ya serikali jumuishi.

Mulembe, ni jina la majazi linalotumika kutambua jamii ya eneo la Magharibi mwa Kenya, Waluhya.

Bw Oparanya ni kati ya mawaziri ambao wanatoka mrengo wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga ambao walinufaika kutokana na mabadiliko ya mwezi uliopita, Julai 2024, kwenye baraza la mawaziri.

“Sisi kama watu kutoka eneo la Magharibi hatujanufaika ilhali baadhi ya viongozi wetu wamekuwa wakisema wapo serikalini. Bw Oparanya naomba utumie wadhifa huu kuleta mabadiliko eneo letu,” akasema Bw Aladwa.

Alikuwa akizungumza kwenye ibada katika kanisa moja Makadara, maombi ambayo yalihudhuriwa pia na Bw Oparanya mwenyewe.

“Tafadhali saidia makundi ya akina mama na vijana kwa sababu wizara unayoshikilia ina umuhimu sana. Uwepo wapo serikalini unastahili kuhisiwa kupitia miradi ya maendeleo,” akaongeza mbunge huyo wa ODM.

Bw Aladwa alisema wanasiasa wa Magharibi wanaohudumu kwenye baraza la mawaziri hawafai kulala kazini na kwamba wanapaswa kumuiga Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye amekuwa akiwatetea sana wakazi wa Mlima Kenya.

“Gachagua amekuwa akisema serikali hii ni ya hisa. Hisa ya watu wa Magharibi ni hizi wizara mnazoshikilia,” akasema.

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula wanaotoka eneo hilo, wamekuwa wakikashifiwa kwa kutofanya chochote kuhakikisha wanainua maisha ya wakazi wa eneo la Magharibi.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo