Habari za Kitaifa

Miradi ya Sh12 bilioni imekwama katika kaunti 10 – Ripoti

Na ERIC MATARA August 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UTEKELEZAJI wa miradi ya thamani ya Sh12 bilioni katika kaunti 10 nchini, ambayo ingeimarisha maisha ya wakazi na uchumi wa kaunti hizo, zimekwama na kuanika hali mbaya ya maendeleo katika maeneo husika.

Ripoti ya hivi punde ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu imeonyesha kuwa licha ya mabilioni ya pesa za umma kuwekezwa katika miradi hiyo, imetelekezwa hali ambayo inaibua maswali kuhusu jinsi pesa hizo zilivyotumika.

Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa vituo vya kiafya, barabara, madarasa katika shule za chekechea (ECDEs), makazi ya magavana na manaibu wa magavana, viwanja vya michezo, miongoni mwa miradi mingine.

Kaunti ambazo kuna miradi isiyokamilika, kulingana na ripoti hiyo ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma ndani ya mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2023 ni; Nairobi, Kiambu, Baringo, Nakuru, Turkana, Pokot Magharibi, Tana River, Kitui, Nyamira na Trans Nzoia.

Miradi hiyo iliyokwama, ilitelekezwa baada ya kukamilishwa, au kukamilishwa kwake kulicheleweshwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kutolipwa kwa wanakandarasi, matumizi ya wanakandarasi wasio na uwezo, mivutano kuhusu zabuni, miongoni mwa sababu nyinginezo.

Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa miradi ya thamani ya Sh1.36 bilioni iliyokwama, ikifuatwa na Kiambu yenye miradi ya thamani ya Sh1.23 bilioni ambayo haikuwa imekamilika.

Katika Kaunti ya Nairobi, nyingi za miradi iliyokwama ni ya hospitali iliyoanzishwa na serikali za kaunti.

“Ukaguzi wa miradi iliyotekelezwa na Serikali ya Kaunti ya Nairobi unaonyesha kuwa miradi ya thamani ya Sh1.36 bilioni ya ujenzi wa hospitali mbalimbali ilikwama,” ripoti hiyo inaeleza.

Kwa mfano, ripoti hiyo inafichua kuwa ujenzi wa uwekaji vifaa katika Zahanati ya Pumwani Lucky Summer, ujenzi na uwekaji vifaa katika Kituo cha Kiafya cha Pumwani Majengo na ujenzi na uwekaji vifaa katika Zahanati ya Gumba/Mabatini ilikwama.

“Ukaguzi ulioendeshwa katika miradi hii mnamo Septemba 28 na Septemba 29, 2023 ulionyesha kuwa haikukamilika. Aidha, ujenzi wa ua la kuzingira Kituo cha Afya cha Pumwani Majengo na ua la kuzingira Zahanati Lucky Summer ulianza na haujakamilika na sasa uko katika hali mbaya,” ripoti hiyo inaeleza zaidi.

Vilevile, licha ya kutokamilishwa kwa miradi hiyo, mwanakandarasi huyo huyo alipewa zabuni nyingine ya Sh 344,100,000 kutekeleza ujenzi wa awamu ya 11 katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki.

Mradi huo pia ulikwama baada ya Sh165,099,105, kulipwa na serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Katika Kaunti ya Kiambu inayoongozwa na Gavana Kimani Wamatangi, miongoni mwa miradi iliyokwama ni ujenzi wa jengo la ghorofa nne katika Hospitali ya Level 4 ya Bibirioni kwa gharama ya Sh285.99 milioni.

Miradi mingine ni ujenzi wa wadi yenye ghorofa tatu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Tigoni kwa gharama ya Sh160.74 milioni na ujenzi wa wadi ya ghorofa nne katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Lari kwa gharama ya Sh191.80 milioni.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo