Lugha, Fasihi na Elimu

Matumizi yasiyo sahihi ya msamiati ‘mahame’ na ‘salia’ (sehemu 1)

Na ENOCK NYARIKI August 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MCHANGO wa vyombo vya habari katika kuunda na kusambaza istilahi na msamiati katika ulimwengu unaoendelea kwa kasi kiteknolojia ni wa kupigiwa mfano.

Hata hivyo, vyombo hivyo pia hupotosha umma kwa kutumia baadhi ya dhana visivyo. Miongoni mwa dhana ambazo zimekuwa zikikosewa kimatumizi ni ‘mahame’ na ‘salia’.

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, nitaangazia neno ‘mahame’ ijapokuwa yote mawili yaani ‘mahame’na ‘salia’ aghalabu hutumiwa pamoja.

Neno ‘mahame’ hutumiwa na vyombo vya habari kurejelea hali ya kutokuwepo kwa watu au kuwepo kwa watu wachache sana mahali fulani –pawe sokoni, madukani, barabarani, njiani,uwanjani, kanisani n.k.

Neno ‘salia’ ambalo tutalijadili kwa kina katika makala yajayo, nalo hutumiwa kwa maana ya kubadilika ghafla na kubaki hivyo kwa muda fulani. Maneno haya mawili yanapotumiwa pamoja huchora taswira ya hali ya kutokuwepo (kwa muda fulani) watu mahali ambapo watu wengine wamezoea kuwaona.

Neno ‘mahame’ limeundwa kutokana na kitenzi ‘hama’ chenye maana ya kuondoka katika maskani yako na kuenda kuishi mahali pengine.

Kwa mintarafu hii, makazi au mahali palipohamwa na kubaki patupu ndipo mahame. Nonimo ‘mahame’ imefikiwa kwa kuhusisha michakato mbalimbali.

Kwanza, kuna matumizi ya kiambishi {e} mahali pa {a} ambacho kimsingi si sehemu ya mzizi wa kitenzi husika. Kiambishi {e} hutekeleza dhima mbalimbali kisarufi zikiwamo kuamrisha, kutoa rai na kuonyesha kauli.

Kwa hivyo, kwa kutumia kiambishi {e} kitenzi ‘hama’ kinanominishwa kuwa ‘hame’.

MAKALA YATAENDELEA…