Ushahidi wa nyama ya mbwa iliyooza waharibiwa kortini
Na RICHARD MUNGUTI
NYAMA ilizoozea ndani ya nyumba ya raia watatu wa Uchina walio kizuizini na kuchafua hewa katika wa mtaa wa kifahari wa Kilimani, Nairobi iliharibiwa Alhamisi.
Hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Bw Kennedy Cheruiyot aliyeenda kupokea ushahidi kuhusu nyama hizo zaidi ya kilo 500 aliwaamuru maafisa wanaohusika na afya ya umma waziharibu kwa kuzichoma.
Waliofika kwenye nyumba ya Wachina hao walishika mapua huku wakitia vitambaa lakini hilo halikusaidia chochote kwani uvundo ulipenyeza na kufanya wengi waliofika kuhisi kutapika.
Maafisa wa polisi walioandamana na Bw Cheruiyot kupokea ushahidi huo walivumilia hata ikabidi mmoja aseme, “Kweli kazi ya polisi ni utumishi wa wote.”
Akisema hayo maafisa wa idara ya Afya ya Umma walikuwa amevalia vichungi kwenye mapua kujizuia.
Hata hivyo hakimu alipokea ushahidi huo na kuamuru nyama hizo ziharibiwe kabisa.
Bw Cheruiyot alienda kwa makazi ya Bi Shang Li Yan baada ya maafisa wa idara ya umma kusema “uvundo unaotoka kwenye makazi ya raia hao wa Uchina umewafanya wakazi wengi kuhama.”
Kiongozi wa mashtaka aliambia mahakama kuwa “hali imekuwa ngumu kwa wakazi wa mtaa wa Kilimani.
Korti ilifahamishwa tangu raia hao watatu wa Uchina watiwe nguvuni na kuzuiliwa korokoroni , eneo la Aberdare mtaani Kilimani imekuwa kama kichinjio kwa sababu ya uvundo kutoka kwa nyumba ya wakazi hao.
Bi Yan alishtakiwa kwa makosa ya kupika chakula cha kuuza katika mazingira yasiyo safi.
Katika nyumba yake maafisa wa idara ya afya kwa umma walipata kilo 95 za nyama nyekundu, kilo 130 za samaki, nyama za Nguruwe na nyama nyinginezo kilo 285.
Pia alishtakiwa kupatikana na makatoni tano ya Samaki waliohifadhiwa kwenye mikebe ya gramu 250 ambayo muda wake wa kuuzwa ulikuwa umeyoyoma.
Kiongozi wa mashtaka alipinga Bi Yan akiachiliwa kwa dhamana akisema “bado anaendelea kuchunguzwa kwa makosa mengine pamoja na raia wengine wawili wa Uchina na Mkenya mmoja aliyedai ameajiriwa kazi na Bi Yan.”
Mawakili Assa Nyakundi na Bw David Ayuo wanamwakilisha Bi Yan. Bw Nyakundi hakupinga ombi la kuharibiwa kwa nyama hizo.
“Nataka kuieleza mahakama hii kuwa Polisi wamesababisha habari zilizowaharibia majina na sifa washukiwa hawa watatu kwa kudai walikuwa wanauza na nyama za mbwa,”akasema Bw Nyakundi.
Akaongeza kusema, “Msemo kuwa kile kilichosumu kwa mmoja ni kitamu kwa mwingine umetimilika. Sio jambo fiche kwamba kuna makabila ulimwenguni wanaofurahia minofu ya nyama za mbwa na hata wengine huchagamkia nyama ya sokwe, tumbili, nyoka, panya na hayawani wengineo. Kupatikana na nyama za mbwa sio hatia.”
Wakili huyo aliendelea kusema kuwa yuko na ushahidi wa risiti kwamba nyama hizo zilikuwa zimenunuliwa kutoka Supa na Buchari.
“Wakati ukiwadia wa kesi hii kusikizwa nitatoa ushahidi mkamilifu kuhusu nyama hizi,” akasema Bw Nyakundi.
Wakili huyo hakupinga mashtaka yakiwasilishwa dhidi ya mshtakiwa huyo.
Bi Yan, Xing Wei, Zhang Jie na Bw David Maseno Oseko walizuiliwa hadi Januari 14 kusaidia polisi kukamilisha uchunguzi.
Washukiwa hao waliamriwa wawekwe rumande Jumatano na hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe alipofahamishwa washukiwa wanahojiwa kwa kupatikana na Kombe na bidhaa za wanyama wa Pori.
“Washukiwa wanaendelea kuchunguzwa kwa makosa mengine na Bi Yan atarudishwa korokoroni kuendelea kuchunguzwa pamoja na washukiwa wengine hadi wiki ijayo,” hakimu alifahamishwa.