Dili ya Merino kuja Arsenal imeshika karibuni itaiva
ARSENAL imeimarisha juhudi zake za kumsajili Mikel Merino kwa kuanzisha rasmi mazungumzo na Real Sociedad ambayo yanatarajiwa kufaulisha uhamisho huo.
Mnamo Alhamisi, Mkurugenzi wa Michezo Arsenal Edu Gaspar alisafiri hadi Uhispania kukutana na wamiliki wa Real Sociedad kukamilisha dili hiyo.
Mashabiki wa Arsenal walikuwa wamekata tamaa jinsi mchakato wa kusajili raia huyo wa Uhispania ulikuwa ukiendeshwa kwa mwendo wa kobe huku klabu zingine zikianza kummezea mate.
Merino, 28, angependa kuchezea Arsenal na pia Sociedad imesema kuwa ipo tayari kumuuza mwanadimba huyo ambaye yupo kwenye mwaka wa mwisho katika mkataba wake na klabu hiyo.
Klabu yoyote ambayo ingetaka kupata saini ya Merino inastahili kulipa Sociedad Sh9.3 bilioni, kwa mujibu wa makadirio ya thamani yake sokoni kwa sasa.
Hata hivyo, ripoti kutoka Uhispania zinasema kuwa Sociedad inaweza kukubali kati ya Sh4.1 bilioni hadi Sh5 bilioni kwa mwanadimba huyo.
Arsenal ingependa kumsajili kiungo huyo kabla ya msimu wa uhamisho wa wanasoka kukamilika mnamo Agosti 30 na Edu amekuwa Uhispania tangu Alhamisi kusuka dili hiyo ili ikamilike mara moja.