Magufuli aungama anasikiliza simu na kusoma SMS za mawaziri wake
THE CITIZEN NA PETER MBURU
RAIS wa Tanzania John Pombe Magufuli Jumatano alitangaza kuwa amekuwa akifuatilia mawasiliano ya simu ya maafisa wa serikali yake ili kuchunguza uhusiano wao wa kikazi, akiwarai kuinua viwango vyao vya uongozi.
Rais Magufuli alisema kuwa hatua yake ya kumuajiri Dkt Zainab Chaula kuwa katibu katika wizara ya afya ilichochewa naye kufuatilia mawasiliano ya simu kati yake na waziri wa afya Ummy Mwalimu.
Rais huyo alisema haya wakati wa hafla ya kulisha kiapo mawaziri wapya, makatibu wa kudumu na maafisa wengine wakuu serikalini.
“Nilipofuatilia mawasiliano ya jumbe fupi kwa simu kati ya Waziri wa Afya na Dkt Chaula (ambaye alikuwa naibu katibu wa serikali ya wilaya na msimamizi wa afya wa eneo), nilibaini kuwa kulikuwa na tatizo katika ushirikiano wao wa kikazi. Ili kumaliza migogoro baina yao, niliamua kuwaweka katika wizara moja,” akasema Bw Magufuli.
“Mnapochukua majukumu yenu mapya, mtakumbana na majaribio mengi,” Rais huyo akaonya maafisa hao wa serikali, katika hafla hiyo iliyofanyika Dar es Salaam.
Alisema kuwa kuna mizozo kuhusiana na baadhi ya maamuzi katika wizara fulani za serikali, ikihusisha mawaziri, makatibu na viongozi wa mikoa na wilaya.
“Ninawatazama. Hili lazima liishe,” akasema.
Jumanne, Rais huyo alifanya mabadiliko ya wizara ambapo alimwondoa waziri wa madini Angellah Kairuki na kmhamishia afisi ya Waziri Mkuu, kisha kumpa Dotto Biteko aliyekuwa naibu wa waziri kazi hiyo.
Aidha, alifanya mabadiliko kwa makatibu wa wizara tofauti na mabalozi.