Habari za Kitaifa

Ngome ya Raila taabani wanasiasa waking’ang’ania uongozi wa chama  

Na GEORGE ODIWUOR August 19th, 2024 1 min read

KINARA wa ODM Raila Odinga huenda akalazimika kuzuru Kaunti ya Homa Bay ili kutatua mzozo wa uongozi wa chama hicho kwenye gatuzi hilo.

Wanasiasa katika eneo hilo wanapigania kuongoza chama hicho cha chungwa, jambo ambalo linatishia kuleta mgawanyiko miongoni mwao na wafuasi wengine kwa ujumla.

Wabunge wasiopungua watano wameonyesha nia ya kuwa mwenyekiti wa chama na hakuna aliye tayari kuachilia azma yake kwa mwingine.

Wanaomezea mate nafasi hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kasipul Ong’ondo Were, mwenzake wa Homa Bay Town Peter Kaluma, Mbunge wa Karachuonyo Adipo Okuome na mwenzake wa Ndhiwa Martin Owino.

Seneta Moses Kajwang, Mwakilishi wa Wanawake Joyce Osogo na aliyekuwa Naibu Gavana Hamilton Orata pia wanawania nafasi hiyo.

Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya Gavana Gladys Wanga ambaye alihudumu katika wadhifa huo kuanzia 2016 kupandishwa hadhi na kuwa mwenyekiti wa kitaifa wa ODM.

Alichukua nafasi ya John Mbadi ambaye aliteuliwa na Rais William Ruto kuwa Waziri wa Fedha katika serikali yake “pana.”

Kuachwa wazi kwa kiti cha kaunti kulifungua milango kwa viongozi wengine kupanua taaluma zao za kisiasa.

Lakini pia imesababisha uhasama kati ya wanasiasa wanaomezea mate kiti hicho.

Wafuasi wao na maafisa wa chama, pia wamekuwa na maoni tofauti kuhusu nani anafaa kuongoza.

Ubabe huo unaelekea kuwa kama ule wa 2015 ambapo makundi hasimu yalijitokeza na kuanza kufungua afisi kinzani za chama hicho.

Ilimbidi Bw Odinga kuingilia kati na kufanya mkutano na wanasiasa hao kutatua tofauti zao.

Bw Odinga aliwapa kila mmoja wao majukumu tofauti chamani.

Wafuasi wa wanaomezea mate wadhifa huo wa mwenyekiti, wamekuwa wakifanya mikutano ya kushawishi au kuashiria kuwa ni wafaafu kukirithi kiti hicho.

 Imetafsiriwa na Wycliffe Nyaberi