Dimba

Mkae mkijua taji la tano bado ni letu, Man City waambia Arsenal, Liverpool na Man U

Na MASHIRIKA August 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, Uingereza

KOCHA Pep Guardiola amesema kuwa vijana wake wa Manchester City walicheza kama mabingwa baada ya kubomoa Chelsea 2-0 katika mechi ya kwanza wanapofukuzia taji la tano mfululizo kwenye Ligi Kuu.

Ingawa amekiri ushindani mkali katika vita vya kuwania taji msimu huu wa 2024-2025 utatoka kwa Arsenal, Liverpool, Manchester United na Chelsea, Mhispania huyo alifichua kuwa hakutarajia kabisa City kunyamazisha vijana wa kocha Enzo Maresca ugani Stamford Bridge.

City walishinda mechi hiyo yao ya 16 ya kuanza msimu kati ya 28 kupitia mabao ya Erling Haaland na Mateo Kovacic.

Brighton, Arsenal, Liverpool, Aston Villa, Brentford, Manchester United na Newcastle pia walifungua msimu kwa ushindi.

Licha ya kuwa bila kiungo muhimu Rodri nao Phil Foden, John Stones, Kyle Walker na Nathan Ake walianza kutoka benchi, City walifuatiliza ushindi wa Kombe la Ngao kwa kunyamazisha Chelsea na kumpa Guardiola furaha tele.

“Sikutarajia kabisa. Najua vile vijana wangu wanaweza kufanya, lakini nashangaa katika siku ya kwanza na pia bila kufanya mazoezi.

Nakumbuka msimu jana hatukuweza kupata ushindi Stamford Bridge kwa hivyo ni dalili nzuri. Ni hatua kubwa tumepiga mbele. Ubaya tu ni kuwa bado michuano inasalia mingi, lakini kuanza msimu kwa kushinda kunatuongeza motisha,” akasema Guardiola.

Mhispania huyo alikiri kuwa wako juu kidogo ya wapinzani wengine kutokana na kuwa wamekuwa pamoja kwa misimu tisa kwa hivyo wanajuana vyema.

“Wote ni rafiki, familia zao pia ziko nao mara nyingi. Hiki ni kitu kinanifurahisha sana,” akasema Guardiola na kuwataka wachezaji wake waendelee kukaza kamba katika msimu unaoweza kuwa mrefu zaidi baada ya Klabu Bingwa Duniani kupanuliwa kutoka timu saba hadi 32 mwaka 2025.

Haaland sasa ana mabao 64 kutokana na kuchezea City mara 67 ligini.

City watakuwa wenyeji wa washiriki wapya Ipswich Town hapo Jumamosi.

Chelsea watavaana na Servette katika mkondo wa kwanza wa Europa League Conference ugani Stamford Bridge hapo Alhamisi kabla ya kurejelea majukumu ya ligi dhidi ya Wolves ugenini Jumapili.