Makala

Mpango kupiga jeki kina mama kuendeleza ufugaji kuku

Na SAMMY WAWERU August 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SAFARI ya Lucy Wanjiru kubadilisha maisha yake ni ya kusisimua, ikiashiria umuhimu wa uvumilivu katika kila jambo.  

Akiwa mkazi wa Wadi ya Riabai, Kaunti ya Kiambu, amepitia changamoto nyingi kujiendeleza kimaisha – ili kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi.

Hata hivyo, maisha yake yalibadilika ghafla kupitia kuzinduliwa kwa mpangu wa Serikali ya Kaunti ya Kiambu kuinua kina mama wanaoendeleza ufugaji wa kuku.

Wanjiru hakujua kuhudhuria mkutano mmoja wa Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi ungebadilisha maisha yake.

Gavana Wamatangi alizindua mpango wa kilimo kupiga jeki wakulima Kiambu, unaolenga sana kina mama kufanikisha kilimo-ufugaji-biashara.

Akiwa mwingi wa matumaini, Wanjiru hakupoteza fursa hiyo.

Alihudhuria mkutano ambapo Gavana Wamatangi alikuwa akisambaza vifaranga wa kuku wa kienyeji walioboreshwa (improved kienyeji chicken) na walioanguliwa kupitia Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro).

Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi akisambaza vifaranga wenye umri wa mwezi mmoja katika Kaunti Ndogo ya Kabete. PICHA|SAMMY WAWERU

Wanjiru aliposkia kuhusu usambazaji wa vifaranga hao bila malipo, aliandamana na wakazi kadhaa wa eneo anakoishi.

Alikuwa mwingi wa subira, na baada ya hotuba kadhaa ukawadia wakati aliongojea kwa hamu na ghamu.

Akimpa motisha, Gavana Wamatangi alimkabidhi vifaranga waliowekwa kwenye katoni.

Alirejea nyumbani akiwa amejawa na furaha.

“Ni vigumu sana nikihudhuria mikutano ya hadhara, hata ikiandaliwa nje ya boma langu. Lakini mkutano wa Gavana niliuhudhuria. Nilirejea nyumbani nikiwa na matumaini makuu kwa kupewa vifaranga, na miezi sita baadaye ninaridhia hatua nilizopiga,” Wanjiru anasema.

Kwenye mojawapo ya sehemu ya boma lake, ndiko anaendeleza ufugaji wa kuku.

Kando na ukarimu wa Serikali ya Kaunti ya Kiambu chini ya Bosi wake Kimani Wamatangi, amenufaika pakubwa kupitia ushauri nasaha jinsi ya kufuga kuku kupitia kwa maafisa wa idara ya ufugaji katika serikali hiyo.

Alianza na idadi ndogo ya vifaranga, na sasa anajivunia kuuza mayai.

Safari ya Wanjiru ni kioo cha mamia ya wanawake wengine Kiambu waliofaidika kupitia mpango wa Serikali ya Kaunti ya Kiambu kuwapiga jeki.

Lucy Wanjiru, mmoja wa wafugaji Kiambu waliopewa vifaranga wa umri wa mwezi mmoja kupitia Serikali ya Kaunti ya Kiambu. PICHA|SAMMY WAWERU

Kila mmoja akiwa alitunukiwa kuku 10 na wengine 5, wanawake hao sasa wanamudu kutafutia familia zao riziki.

Florence Waithera, mkazi wa Ndumberi, ni miongoni mwa wanawake 34, 000 Kiambu waliopata jumla ya vifaranga 200, 000 waliosambazwa tangu program hiyo kuanzishwa.

Waithera anasema amechanganya vifaranga aliopewa na wake halisi wa kienyeji.

“Bridi hii inakua haraka na nilianza kukusanya mayai wiki chache baada ya kuwapokea,” akaambia Taifa Dijitali ilipomtembelea nyumbani kwake Ndumberi.

Aidha, alitunukiwa vifaranga 5 na chini ya miezi sita pekee ametinga kuku 50.

Lucy Wanjiru akilisha kuku aliopewa na Serikali ya Kaunti ya Kiambu. PICHA|SAMMY WAWERU

Mama mwingine ni Regina Wairimu, ambaye ni mkazi wa wadi ya Kiambu Township, anayesifia kuku hao wa kisasa kukua haraka na wanaostahimili magonjwa ya ndege.

“Kinyume na kuku niliokuwa nikifuga, niliopewa na Serikali ya Kaunti ya Kiambu wanahimili baridi,” Wairimu anasema.

Mpango wa usambazaji kuku Kiambu, Gavana Kimani Wamatangi aliuzindua Julai 2023.

Ni mojawapo ya sera zake kusaidia Rais William Ruto kuafikia ajenda kuinua uchumi kutoka chini kuelekea juu, maarufu kama Bottom-Up Economic Transformation Agenda (BETA).

Dkt Ruto amekuwa akisisitiza haja ya kupiga ya kupiga jeki sekta ya kilimo na ufugaji, ili kuangazia uhaba wa chakula nchini.

Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi akisambaza vifaranga wenye umri wa mwezi mmoja kwa wafugaji wa kuku eneo la Juja. PICHA|SAMMY WAWERU