• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
UPWEKE: Ruto aachwa kujipigania hadi 2022

UPWEKE: Ruto aachwa kujipigania hadi 2022

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto anakabiliwa na upweke wa kisiasa baada ya waliokuwa wandani wake kuanza kumhepa na kuanzisha kampeni ya kumwekea vikwazo kwenye azma yake ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Bw Ruto hajaonekana hadharani kwa wiki moja sasa huku cheche za siasa za urithi hasa zinazomlenga zikipamba moto.

Katika ngazi ya juu, dalili ni dhahiri kuwa hali si hali tena jinsi ilivyokuwa kati ya Bw Ruto na bosi wake katika kipindi chao cha kwanza cha utawala, ambapo walionekana mara nyingi hadharani wakipigana pambaja, kucheka na kuhudhuria hafla nyingi kwa pamoja.

Siku hizi kinachoonekana ni kijibaridi na kupungua kwa fursa za wawili hao kujumuika pamoja hadharani. Badala yake kiongozi wa ODM Raila Odinga ndiye amekuwa akitokezea zaidi kwenye hafla za rais na kujumuika naye kwa karibu zaidi.

Rais hajazungumzia kuhusu suala hilo lakini matamshi ya wanasiasa wanaoegemea upande wake yanaashiria mabadiliko ya misimamo.

Matukio ya majuzi nayo yanaonyesha mbinu ya kumtenga Bw Ruto na kumwekea vizuizi kwenye safari yake kuelekea 2022.

Hapo jana viongozi wa wanawake wa Jubilee wakiungwa mkono na wenzao wa ODM walianzisha vuguvugu ambalo walisema ni la kuhimiza uungaji mkono wa mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga na kupinga kampeni za mapema, ambazo Bw Ruto na wandani wake wamelaumiwa kuanzisha.

Kwenye taarifa iliyosomwa na Gavana Anne Waiguru (Jubilee) wa Kirinyaga na Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga, viongozi hao walisema wanamtambua juhudi za Rais Kenyatta na Bw Odinga kukumbatia umoja.

Wakati wa uchaguzi wa 2017, viongozi wa eneo la Mlima Kenya walikuwa kwenye mstari wa mbele kutangaza kuwa jamii ya eneo hilo ingerudisha mkono kwa Bw Ruto 2022 kutokana na mchango wake katika kuhakikisha jamii ya Kalenjin ilisimama stadi nyuma ya Rais Kenyatta kwenye chaguzi za 2013 na 2017.

Katika kila hadhira, viongozi hao, akiwemo rais mwenyewe, walisisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa kipindi chake 2022, watamuunga mkono Bw Ruto kutawala kwa miaka 10.

Lakini wimbo huo sasa umebadilika huku baadhi wakibadili kauli kuwa hakukuwa na mwafaka wowote kuhusu 2022. Hii imesababisha mgawanyiko baina ya viongozi ambao wangali wanamuunga mkono na wale ambao wamebadilisha kauli.

Ndani ya chama tawala cha Jubilee ambapo Bw Ruto ndiye Naibu Kiongozi wake, amekuwa akitengwa na kilele kilikuwa tangazo mwezi uliopita la aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama hicho Bw David Murathe, ambaye amejiuzulu kwa kile anasema ni hatua ya kumwezesha kumzima Naibu Rais asichukue urais.

Mbinu nyingine ambayo inafanya Bw Ruto kuonekana kuwa mpweke ni kampeni kuwa anapinga mwafaka wa Rais na Bw Odinga, ambao umetajwa na viongozi hao kama suluhisho la migawanyiko na siasa za chuki zinazochipuka kila wakati wa uchaguzi mkuu nchini.

Naibu Rais pia amekuwa akilaumiwa na wanaompinga kuwa anahujumu maendeleo kwa kuanzisha kampeni za mapema za 2022. Hii inafanya aonekane kama aliyejitenga na ajenda za serikali na badala yake analenga tu kumrithi rais.

Wakenya sasa wanatarajia kuona jinsi Bw Ruto atakavyopambana na mawimbi ya upinzani yanayotishia kuzima nyota yake.

You can share this post!

Kuria na Kimani Ngunjiri wazidi kupondwa

Wateja wa StandChart kuanza kutoa Sh80,000 kwa ATM

adminleo