Habari Mseto

Uhaba wa dawa za kutibu makali ya Kansa Nyanza

Na RUTH MBULA August 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UKOSEFU wa dawa muhimu ni changamoto kuu kwa wagonjwa wa Saratani katika eneo la Nyanza licha ya magavana wa eneo hilo kujizatiti kujenga vituo vya kutibu ugonjwa huo hatari.

Changamoto hiyo ilijitokeza waziwazi Jumatano, Agosti 21, 2024 Gavana wa Kisii Simba Arati alipofungua rasmi kitengo cha kutibu Saratani katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH).

Wagonjwa wa kansa, watunzaji wao na waliopona baada ya kupata tiba walimwarifu Bw Arati kwamba juhudi zake za kupambana na ugonjwa huo zisiishie katika uzinduzi wa kitengo hicho pekee bali ahakikishe zipo dawa za kutosha.

Walielezea mateso wanayopitia kwa kukosa dawa za kudhibiti makali ya ugonjwa huo katika hospitali za umma na wakamtaka Bw Arati kununua dawa hizo.

Kwa mfano, walitaja dawa ya Tomoxifen inayotumiwa kutibu Kansa ya matiti kwa wanaume na wanawake, wakisema ni nadra kupatikana au haipatikani kabisa.

“Dawa hii ya Tomoxifen haipatikani hapa Kisii na hata katika hospitali nyingine za kaunti za eneo zima la Nyanza. Mara nyingi huwa tunaagizwa kusaka dawa hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH) Eldoret,” akasema mgonjwa mmoja ambaye alimshukuru Gavana Arati kwa kujenga Kitengo cha kutibu kansa katika hospitali ya KTRH.

Mgonjwa huyo vilevile, alieleza kuwa kadi ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) haiwezi kuwasaidia kupata Tomoxifen katika hospitali za kibinafsi.

Sasa wagonjwa hao wanalazimika kusaka dawa sehemu za mbali, hali ambayo inawabebesha gharama kubwa.

“Ugonjwa huu umetufyonza rasilimali. Tumesalia maskini hohehahe,” akasema mgonjwa huyo, aliyeomba tubane jina lake.

Dkt Bahati Riogi, mtaalamu wa Kansa na msimamizi wa kitengo cha kushughulikia ugonjwa huo hospitalini KTRH, alithibitisha uwepo wa tatizo la uhaba wa dawa.

“Dawa ya Tomoxifen, ambayo mgonjwa anafaa kumeza kila siku kwa kati ya miaka mitano na 10, huimarisha afya ya mgonjwa anayeugua Kansa ya matiti. Dawa hiyo inagharimu Sh300 katika maduka ya dawa kwa muda wa mwezi mmoja. Bei hiyo inaonekana nafuu. Lakini ukipiga hesabu Sh300 kwa miezi 12 na miaka 10 ni pesa nyingi zaidi kwani wagonjwa hao pia wanakumbwa na gharama nyingine maishani,” akasema.

Dkt Barasa alieleza kuwa kuletwa kwa dawa hiyo karibu na watu katika vituo vya kiafya kutawafaa zaidi wagonjwa wa Saratani.

Kwa upande wake, Gavana Arati aliahidi kununua dawa hizo na kuzisambaza katika vituo vya afya katika kaunti hiyo.