Serikali kutathmini deni la Sh2b kufichua wanakandarasi hewa
Na CHARLES WANYORO
SERIKALI ya Kaunti ya Meru itathmini upya deni la Sh2 bilioni inazodaiwa na wanakandarasi kabla ya kuwalipa.
Naibu Gavana Titus Ntuchiu alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa kaunti haipotezi fedha kulipia miradi hewa.
“Tutahakikisha kuwa tunabainisha gharama ya kila huduma na bidhaa zilizotolewa. Miradi hewa na kandarasi ambazo gharama yake imeongezwa kupita kawaida hazitalipiwa,” akasema.
Akizungumza alipokutana na wahasibu wa serikali wanaokagua madeni ambayo kaunti ya Meru inadaiwa na wakandarasi, Bw Ntuchiu alisema kuwa serikali ya kaunti imebaini kuwa baadhi ya miradi ilitozwa fedha maradufu na wakandarasi.
Alisema baadhi ya miradi pia ilitelekezwa na wakandarasi na haijakamilika kufikia sasa.
Alisema serikali ya kaunti imeunda jopokazi la kuchunguza kandarasi zote zilizotolewa na gavana wa zamani Peter Munya, ambaye sasa ni waziri wa Biashara.
Naibu Gavana ambaye pia ni waziri wa Fedha, alisema kuwa madeni yote halali yatalipwa.
Alisema serikali ya kaunti itaanza kulipa wakandarasi baada ya Hazina Kuu ya kitaifa kutoa fedha.
“Serikali ya Kaunti ilibaini kuwa baadhi ya wanakandarasi waliotoa huduma na bidhaa waliongeza gharama maradufu. Tutawalipa wanakandarasi wote waaminifu waliofanya kazi kulingana na maafikiano,” akasema Bw Ntuchiu.
Wakati huo huo, Bw Ntuchiu aliitaka Hazina Kuu ya Kitaifa kutoa fedha kwa kaunti mapema ili kuepuka mrundiko wa madeni.
“Baadhi ya wanakandarasi wamechukua mikopo kuendesha biashara zao. Ni jambo la kutia moyo kwamba Rais Uhuru Kenyatta ameagiza madeni yote yalipwe,” akasema.