Habari za Kaunti

Waliovamia hafla ya mbunge Kisii kuona cha mtema kuni

Na RUTH MBULA August 26th, 2024 1 min read

POLISI katika Kaunti ya Kisii wanachunguza kisa cha Jumatatu, Agosti 26, 2024 ambapo genge lililojihami vikali kwa mishale, lilivamia watu na kuvuruga mkutano ambao uliandaliwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi.

Maafisa hao wa usalama walifanikiwa kumnasa mshukiwa mmoja kuhusiana na kisa hicho cha mchana katika eneobunge la Mugirango Kusini.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Etago Laban Omol alisema mtu mmoja alipata majeraha baada ya kupigwa mawe akitorokea usalama wake wakati wa ghasia hizo.

Bw Omol alisema kuwa genge hilo lilivamia hafla hiyo katika Shule ya watu wenye mahitaji spesheli ya Nyakero kisha wakavamia watu na kuangusha mahema.

Hapo ndipo vita vilizuka kati ya genge hilo na wafuasi wa Bi Aburi ambaye alikuwa atoe msaada wa viti vya magurudumu kwa walemavu shuleni humo.”

“Tumemkamata mtu mmoja ambaye anaendelea kuzuiliwa. Atafikishwa mahakamani baadaye. Tumefaulu kuhakikisha utulivu upo,” akasema Bw Omol.

Ubabe wa kisiasa umesababisha visa vya fujo kutokea katika hafla mbalimbali tangu uchaguzi mkuu wa 2022. Inadaiwa wanasiasa wamekuwa wakifadhili fujo hizo ili kuwaengua wapinzani wao kuelekea kura ya 2027.

Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki ametembelea Kaunti ya Kisii mara mbili, ambapo amekuwa akitoa onyo kwa wanasiasa wanaotumia vijana kuendeleza ghasia kwa maslahi yao ya kisiasa.