Sababu za Ruto kuagiza NYS kupokea mafunzo ya kutumia bunduki
SHIRIKA la Huduma kwa Vijana Nchini (NYS) hivi karibuni litashirikisha mafunzo ya kutumia bunduki kwa makurutu wake kufuatia amri ya Rais William Ruto.
Rais mnamo Jumatatu, Agosti 26, 2024 alimwaamrisha Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ashauriane na wenzake; Soipan Tuya (Ulinzi) na Profesa Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani) ili kozi ya matumizi ya bunduki ianzishwe kwenye mtaala kwa makurutu wa NYS.
Mafunzo hayo kwa mujibu wa Rais, yatasaidia vijana kushiriki katika oparesheni za kiusalama maeneo mbalimbali nchini, wakisaidiana na maafisa wa usalama.
“Waziri anayehusika na idara ya NYS anafaa kushauriana na mwenzake wa Ulinzi na Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa mafunzo ya vijana hawa yanashirikisha matumizi ya bunduki.
“Hii itahakikisha kuwa wanashiriki oparesheni za kulinda nchi wanapohitajika kufanya hivyo,” akasema Rais Ruto.
Alikuwa akiongea jijini Nakuru wakati wa kufuzu kwa makurutu wa NYS katika chuo cha mafunzo yao Gilgil.
Kwenye hotuba yake, Rais Ruto alisema serikali yake inamakinikia kuimarisha NYS kuhakikisha kuwa inatekeleza wajibu wake kama tu vyombo vingine vya usalama.
Zaidi ya makurutu 14, 692 walifuzu wakati wa hafla hiyo ambayo ilikuwa ya 88 tangu NYS ianzishwe.
Aidha, kiongozi wa nchi alisema kuwa baadhi ya mageuzi ambayo yamekuwa yakiendelea katika idara hiyo, lazima matokeo yake yahisiwe maeneo mengine ya nchi.
Kati ya mageuzi mengine aliyopendekeza ni kuongeza idadi ya makurutu wanaojiunga na NYS ili kila kaunti ifikiwe nchini na pia kuwe na mpango wa kusawiri shirika hilo kama linalotekeleza wajibu wake tu kama vyombo vingine vya usalama.
“NYS ni kati ya Idara ambazo haziwezi kutelekezwa kwa sababu ya mchango wao katika kutoa huduma kwa raia na usalama wa kitaifa. Jinsi tu serikali itaongeza idadi ya vijana wanaojiunga na jeshi ndivyo pia wale ambao wanajiunga na NYS wataongezwa,” akasema Rais.
Serikali ikilenga kupanda miti bilioni 10 kufikia mwaka 2032, Rais Ruto alisema kuwa makurutu wa NYS watatumiwa kwenye juhudi za kutunza mazingira nchini.
“Maafisa wa NYS watakuwa wakikagua na kufuatilia vijana ambao watakuwa wakipanda miti chini ya vuguvugu la ‘Tabianchi inayofanyakazi Mtaani’ Kenya ikitarajia kuwa nchi kijani kibichi ambapo mazingira yanaridhisha,” akasema.
Wakati wa hafla hiyo, Rais aliamrisha vyombo vyote vya usalama vihakikishe kuwa makurutu wa NYS wanapewa wajibu katika idara ya ulinzi kwa sababu wameonyesha nidhamu na uwezo mkubwa wa kulinda taifa lao.
Kiongozi wa nchi alipongeza makurutu hao baada ya kufuzu na akawataka wayafuate yale ambayo walifunzwa kambini ili waihudumie jamii kwa utaalamu mkubwa.
“Mna sifa ambazo zinahitajika kuonyesha uzalendo na utumishi katika utumishi wa umma. Nchi yenu inatarajia kuwa mtawajibika na tuna imani katika utendakazi wenu,” akasema Rais.