Koma kututishia, wakosoaji wa Gachagua Mlimani wafoka
BAADA ya kusitisha malumbano kwa muda mfupi, washirika wa Rais Ruto katika Mlima Kenya wameanza kumshambulia tena Naibu Rais Rigathi Gachagua, kufuatia kauli yake kwamba wakosoaji wake watakataliwa na wapigakura ifikapo Desemba mwaka huu, 2024.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, Wabunge Mwangi Kiunjuri (Laikipia Mashariki), Eric Wamumbi (Mathira) na Duncan Mathenge (Nyeri Mjini), wamemshutumu Naibu Rais kwa kuwatisha wakosoaji wake ili wamuunge mkono.
Ni onyo la hivi punde la Bw Gachagua kwa viongozi wa eneo hilo ambao ‘hawasikilizi wakazi’ akirejelea wakosoaji wake – kubadili mwelekeo au wakataliwe katika uchaguzi mkuu wa 2027, ambalo limezua malumbano mapya.
“Mimi ni mtu anayezunguka vijijini kusikiliza watu wanavyosema. Ninawahakikishia kuwa wapigakura tayari wamefanya maamuzi kuhusu 2027 na baada ya makataa hayo, watawakataa (wale ambao hawatakuwa upande wao),” Bw Gachagua alisema akiwa katika ziara Kaunti ya Kiambu majuzi.
Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali mnamo Jumatatu, Agosti 26, 2024, Bw Ichung’wa alimlaumu Naibu Rais kwa kutisha wakosoaji wake ili kuwaingiza baridi wamuunge mkono kwa kisingizio kwamba anapigania maslahi ya watu wa eneo la Mlima Kenya.
“Vita vyake na wale anaochukulia kuwa karibu na rais kuanzia mabloga na viongozi wengine, vinatokana na kukataa kumuunga kutumia watu kama chombo cha kujadiliana na rais,” alisema Bw Ichung’wa.
Bw Kiunjuri alisema watu wa Mlima Kenya watawahukumu viongozi kulingana na utendakazi wao na wala sio uaminifu wao kwa Bw Gachagua.
“Anaendeleza siasa za upinzani kwa kupigana na serikali ya Ruto na ana ajenda moja tu ya kuwa mfalme wa Mlima Kenya. Tayari tuko serikalini na yeye ni naibu rais, kwa hivyo kama anataka kugombea urais 2027, atuambie na tutafurahi na kumuunga lakini kama hatagombea na bado anataka kuwa mgombea mwenza wa mtu, anapaswa kuwa na subira,” akasema Bw Kiunjuri.
Bw Wamumbi alisisitiza kwamba hawatakubali vitisho vya naibu rais.
“Gachagua si Mungu. Haamui hatima ya viongozi wengine. Tulikuwa na Uhuru, ambaye alitishia viongozi kushoto, kulia na katikati lakini akashindwa kwa kishindo. Anafaa kuwashauri viongozi vijana, sio kuwatisha,” akasema Bw Wamumbi.
Naye Bw Mathenge, alitaja kauli ya Bw Gachagua kama “jaribio la kututisha kuelekea 2027”.
“Ana kura moja. Tunahitaji mwongozo wa maendeleo ya eneo hili unaoelezea kile ambacho amefanikisha katika miaka miwili iliyopita ambayo amekuwa afisini na anachopanga kwa miaka mitatu iliyosalia,” Bw Mathenge alisema.
Bw Dennis Itumbi, aliyekuwa mwanamikakati wa mitandao ya kijamii wa Rais Ruto ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Uchumi bunifu na Miradi Maalum wiki jana, amekuwa akilaumiwa na naibu rais kufuatia uhusiano wake wa karibu na baadhi ya viongozi vijana kutoka eneo la Mlima Kenya akiwemo Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro.
“Naweza kuthibitisha nimekuwa na mikutano mingi na naibu rais kupanga mambo mengi. Maudhui ya baadhi ya mikutano hiyo tangu awe naibu rais ni ya siri, na mengine ni ya vitabu ambavyo huenda tukachapisha siku moja au hata sinema. Kwa sasa, hilo ndilo ninaloweza kusema,” Bw Itumbi aliambia Taifa Dijitali mnamo Jumatatu.
Msemaji wa Naibu Rais, Bi Njeri Rugene, hata hivyo, alikanusha madai kwamba alitoa makataa kwa viongozi wa Mlima Kenya.
“Naibu wa Rais hajatoa makataa kwa yeyote. Amewashauri tu viongozi kusikiliza watu wanavyotaka,” Bi Rugene alisema.
Gavana wa Nyeri Kahiga Mutahi, mtetezi mkuu wa Bw Gachagua, anahoji kuwa baadhi ya viongozi vijana kutoka eneo la Mlima Kenya, wakiwemo wanamikakati wa Rais Ruto, wasaidizi wa karibu wa Rais Ruto na vile vile kundi la magavana wanawake lililopewa jina la G7 linaloongozwa na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, ni baadhi ya makundi makuu yanayopinga Naibu Rais.
Alipoulizwa kutoa maoni yake, Bi Waiguru alijibu tu kwa kusema: ‘Anahitaji Yesu.’
Imetafsiriwa na Charles Wasonga