Habari za Kitaifa

Viwanda vya kibinafsi vyamulikwa kwa kuharibu ubora wa chai

Na VITALIS KIMUTAI August 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI kwa ushirikiano na Bodi ya Majani Chai Nchini (TBK) imeanzisha kampeni ya kuimarisha ubora wa majani chai yanayozalishwa nchini.

Katibu wa Wizara ya Kilimo Paul Rono na Afisa Mkuu Mtendaji wa TBK Willy Mutai wamesema shughuli ya kuchunguza upya taratibu za utoaji leseni kwa viwanda vya kibinafsi vya majani chai itaanzishwa kwa lengo la kuimarisha ubora wa bidhaa hiyo.

Hayo yanajiri baada ya Gavana wa Bomet Hillary Barchok, mwenzake wa Kericho Dkt Eric Mutai na Naibu Mwenyekit wa Shirika la Ustawi wa Majani Chai Nchini (KTDA) kufanya mkutano mjini Bomet kujadili njia za kuimarisha mapato ya wakulima wa zao hilo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wakurugenzi kutoka zoni nane za KTDA na madiwani kutoka maeneo kunakokuzwa majani chai kwa wingi.

“Tunaaangalia upya masuala ya utoaji leseni kama sehemu ya utekelezaji wa mageuzi katika sekta ya majani chai kuhakikisha kuwa viwango vya ubora vinavyozingatiwa na viwanda vya KTDA katika ununuzi wa majani chai mabichi pia vinazingatiwa na viwanda vya kibinafsi kote nchini,” Dkt Ronoh akasema.

“Sharti tuhakikishe kuwa ubora wa majani chai unadumishwa katika ngazi zote za utayarishaji zao hili. Hiyo ndio itatuwezesha kuendelea kushikilia rekodi ya kuwa miongoni mwa mataifa yanayouza nje majani chai kwa wingi na kutuletea fedha nyingi za kigeni,” Dkt Ronoh akaeleza wakati wa mkutano na wakurugenzi wa KTDA na wakulima katika kiwanda cha majani chai cha Tirgaga, Kaunti ya Bomet.

Bw Mutai (Afisa Mkuu wa TBK) alisema maafisa wa ukaguzi kutoka bodi hiyo wanaendesha kampeni ya maeneo kunakokuzwa majani chai kuwaelimisha wakulima kuhusu haja ya kuzingatiwa ubora katika uzalishaji.

“Aidha, kampeni hiyo inalenga kuhakikisha kuwa viwanda vya kibinafsi havikiuki kanuni kuhusu uzingatiaji wa ubora.” akaeleza.

Bw Mutai alisema TBK imepata habari kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanachuuza majani chai, hali inayochangia wakulima kupata hasara kwa sababu wanapokea malipo duni na hawalipwi bonasi.