Habari za Kitaifa

Soko la nje la Kenya latishiwa na Mpox

Na BARNABAS BII August 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MLIPUKO wa ugonjwa wa Homa ya Nyani (Mpox) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), unatishia soko la nje la Kenya linalokua kwa kasi zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku serikali ikiimarisha uchunguzi ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hatari nchini.

Mauzo ya Kenya kwenda Kinshasa, soko kuu la nje la wafanyabiashara wengi wa Kenya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, yanakabiliwa na mkanganyiko mpya kufuatia uamuzi wa baadhi ya nchi zinazopakana na DRC kuweka vikwazo vikali vya afya ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo wa kutisha.

Wafanyabiashara wanaojishughulisha na bidhaa za kilimo – ngano, samaki, tumbaku na sukari wameelezea hofu ya kupata hasara kubwa baada ya kuzuka kwa ugonjwa huo ambao umeleta pigo kwa soko lao kuu la nje.

“DRC ndio soko letu kuu la nje la samaki na mlipuko wa virusi vya Homa ya Nyani nchini umeathiri vibaya biashara zetu,” John Loiritei wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufuo wa Impressa (BMU) Ziwa Turkana alisema.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza milipuko ya Homa ya Nyani Barani Afrika kuwa dharura ya kimataifa huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiripoti visa vipya zaidi ya 1,000 katika muda wa wiki mbili zilizopita, kuashiria ongezeko la tishio la ugonjwa huo hatari.

Kulingana na Shrika la Takwimu Nchini (KNBS), katika robo ya kwanza ya 2024, mauzo ya Kenya hadi DRC yaliongezeka kwa zaidi ya nusu na kufikia Sh8.62 bilioni katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka.

Mauzo ya nje yaliongezeka kutoka asilimia 7.69 hadi asilimia 10.74, huku bidhaa muhimu kwa soko la nje zikiwa ni unga wa ngano, samaki, tumbaku, vyuma, mafuta ya petroli na sukari.

Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda nchini (KNCCI) kinakadiria mauzo ya Kenya hadi DRC kwa takriban tani 400 kila mwezi zenye thamani ya Sh147.2 milioni na mlipuko wa Homa ya Nyani huenda ukaleta pigo kwa sekta hiyo ndogo.

Wafanyabiashara hao hutafuta samaki wao hasa kutoka maziwa Victoria na Turkana, huku wafanyabiashara wa Kenya wanaofanya shughuli zao katika Mji wa Busia wakisafirisha samaki katika maeneo ya Mashariki mwa DRC inayopakana na Uganda.

Uuzaji wa samaki nje ya nchi unaishia Bukavu, Kisangani, Goma na maeneo mengine ya Mashariki ya miji ya DRC.

“Wafanyabiashara wa ndani wanatumia fursa ya ukosefu wa soko letu kuu nchini DRC kupunja wafanyabiashara wa samaki kwa kununua kwa bei ya chini,” alisema Stephen Ekal Ekuwom, afisa wa BMU Ziwa Turkana.

Ripoti ya tathmini ya biashara ya Tume ya Bahari ya Hindi inaonyesha kuwa DRC inaagiza wastani wa tani 89,000 za samaki hasa kutoka Ziwa Turkana ili kukidhi matumizi yake ya ndani.

“Uzalishaji wa mapato kutokana na samaki kuzunguka Ziwa Turkana ulikuwa umeongezeka kutoka Sh12 milioni hadi Sh16 milioni, huku uzalishaji ukiimarika kutoka tani 31 hadi tani 35 katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Lakini ukosefu wa soko unaweza kurudisha nyuma faida,” alisema Napokol Epat, mfanyabiashara wa samaki, Ziwa Turkana.

Wastani wa kilo 15,000 za samaki zilisafirishwa kutoka Ziwa Turkana hadi soko la Nairobi na 6,000 hadi Kitale kutoka ufuo wa Impressa pekee mwezi uliopita.

Imetafsiriwa na Wycliffe Nyaberi