Habari za Kitaifa

Lenolkulal huenda akawa gavana wa kwanza kusukumwa jela

Na RICHARD MUNGUTI  August 29th, 2024 1 min read

ALIYEKUWA Gavana wa Samburu Moses Kasaine Lenolkulal atakuwa Gavana wa kwanza kusukumwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kupokea kwa njia ya ufisadi kitita cha Sh83 milioni miaka 11 iliyopita.

Hakimu mkuu katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani, Bw Thomas Nzioki alimpata na hatia Bw Lenolkulal kwa mashtaka ya kufanya biashara na kaunti hiyo.

Bw Nzioki alisema makosa aliyofanya Lenolkulal ni kukataa kufichua kwamba kampuni ya kuuza mafuta ya Petroli ya Oryx Service Station ilikuwa biashara yake.

Bw Nzioki alimpata na hatia gavana huyo aliyehudumu kwa miaka 10 katika mashtaka 10 na kumwachilia huru kwa kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote, hii mahakama imewapata na hatia ya kushiriki ufisadi na kutumia vibaya mamlaka mliyokuwa nayo,” alisema Bw Nzioki akiwahukumu.

Lenolkulal na wenzake walipelekwa kuzuiliwa katika Gereza la Viwandani wakisubiri kuadhibiwa na kuelezwa miaka watakayotumikia vifungo Alhamisi, Agosti 29, 2024.

Bw Moses Lenolkulal, Gavana wa zamani Samburu akiwa kortini mnamo Jumatano, Agosti 28, 2024. PICHA|RICHARD MUNGUTI

Walioshtakiwa kwa kutotunza pesa za umma ni Lenolkulal, Stephen Letinina, Daniel Nakuo, Josephine Naamo, Reuben Marumben Lemunyete, Milton Lenolngenje, Paul Lolmingani, Bernard Lesurmat, Lilian Balanga, Geoffrey Barun na Hesbon Wachira Ndathi.

Kwa jumla walikabiliwa na mashtaka 12.

Shtaka lilisema washtakiwa walikula njama za kushiriki ufisadi kati Machi 27, 2013 na Machi 25, 2019 mjini Maralal, Kaunti ya Samburu kwa kulipa kampuniya ya Oryx Sh83, 467, 995.

“Hii mahakama imefikia uamuzi kwamba upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka 11 dhidi ya washtakiwa ya kushiriki ufisadi, kulipa kimakosa pesa za umma na kutumia vibaya mamlaka ya afisi,” alisema Bw Nzioki.

Baada ya kuwapata na hatia, hakimu alifutilia mbali dhamana walizokuwa wamepewa washtakiwa na kuamuru wasukumwe gerezani wakisubiri vifungo.