Makala

Gachagua: Nitahudhuria ‘Birth Day’ ya Ida Odinga Addis Ababa 2025

Na CHARLES WASONGA August 29th, 2024 1 min read

NAIBU Rais Rigathi ameelezea matumaini kuwa maaadhimisho yajayo ya siku ya kuzaliwa ya Mkewe Raila Odinga, Mama Ida Odinga, yatakuwa jijini Addis Ababa, Ethiopia na kwamba atahudhuria.

Akiongea Jumanne, Agosti 27, 2024 katika Ikulu ya Nairobi wakati wa kuzinduliwa rasmi kwa kampeni za Bw Odinga za kuwania cheo cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Bw Gachagua alimsifu Bi Ida kwa kusimama na mumewe nyakati zote; za raha na majonzi.

“Mama Ida tunakuheshimu na kukuenzia kama taifa kwa kuwa nguzo thabiti kwa mumeo. Umesimama naye nyakati ngumu na anapohisi kulemewa,” Bw Gachagua akasema.

“Nakutakia mema unapoadhinisha siku yako ya kuzaliwa. Na ninaamini kuwa maadhimisho yajayo ya siku kama hiyo yatafanyika kule Addis Ababa kwa sababu Raila atashinda kiti cha AUC. Na ewe Rais Ruto, ikiwa hautapata nafasi ya kuhudhuria sherehe hiyo, nitakuwakilisha katika maadhimisho hayo ya siku ya kuzaliwa kwa Mama Ida,” akaeleza huku akiibua kicheko.

Mama Ida aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumamosi, Agosti 24, 2024 ambapo alitimu umri wa miaka 74.

Bw Gachagua alisema mkewe, Pasta Dorcas Rigathi, amekuwa akimwombea Bw Odinga aibuke mshindi katika kinyang’anyiro hicho cha uenyekiti wa AUC.

Uchaguzi huo utafanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia Februari 28, 2025.

Bw Odinga anashindana na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Youssouf, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Mauritius Anil Gayan na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard Randriamandrato.