Harris aendelea kumlemea Trump katika kura ya maoni
MGOMBEA urais wa Amerika, kupitia kwa chama cha Democrat Kamala Harris, anaoongoza mpinzani wake wa Republican Donald Trump kwa umaarufu.
Harris ameandikisha umaarufu wa asilimia 45 kulingana na matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa na shirika la Reuters/Ipsos na kuchapishwa Alhamisi, Agosti 29, 2024.
Trump naye ameandikisha umaarufu wa asilimia 41 katika kura hiyo iliyoendeshwa kitaifa miongoni mwa wapiga kura.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa Makamu wa Rais huyo anaendelea kuibua msisimko miongoni mwa wapiga kura kuelekea uchaguzi wa urais wa Novemba 5, 2024.
Kura hii ya maoni, iliyoendeshwa kwa siku nane ilikamilika mnamo Jumatano, Agosti 28, 2024 na kuonyesha kuwa Bi Harris anapata uungwaji mkono zaidi miongoni mwa wanawake na Waamerika wa asili ya Uhispania.
Tangu Rais Joe Biden, 81, ajiondoe kutoka kampeni za urais Julai 21 na kumpendekeza makamu wake kwa nafasi hiyo, umaarufu wa Harris umekuwa ukipanda katika ngazi ya kitaifa na katika majimbo muhimu ambayo huamua mshindi katika chaguzi za urais nchini Amerika.
Japo kura za maoni za kitaifa kama hii ya Reuters/Ipsos huonyesha hisia za wapiga kura, matokeo ya kura ya wajumbe kutoka majimbo ya Amerika (Electoral College) ndiyo hutumiwa kuamua mshindi wa urais.
Aidha, idadi ndogo za majimbo yenye idadi kubwa ya kura za wajumbe huamua mshindi.
Kwa mfano, katika majimbo saba ambako kulishuhudiwa ushindani wa karibu, Wisconsin, Pennsylvania, Georgia, Arizona, North Carolina, Michigan na Nevada – Trump anaongoza kwa asilimia 45 ya uungwaji mkono huku Harris akiwa na umaarufu wa asilimia 43.
Hali hii ingali inawatia hofu wafuasi wa chama tawala cha Democrat.