Habari za Kitaifa

Ugatuzi katika njia telezi magavana wakinunia serikali kuu

Na SHABAN MAKOKHA August 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UTATA unanukia kati ya serikali kuu na magavana kuhusu mgao wa mapato ya nchi na kucheleweshwa kwa pesa za kufadhili ugatuzi.

Wakuu hao wa kaunti wameonya kuwa huduma za dharura huenda zikakwama kutokana na kuondolewa kwa Mswada wa Fedha 2024 na pia kaunti kuchelewa kupata mgao wao wa kila mwezi.

Wizara ya Fedha imependekeza kuwa kaunti zikatwe Sh20 bilioni kwenye idadi ya jumla ya Sh400.1 bilioni ambazo zinastahili kuelekezewa kaunti 47 mwaka huu wa kifedha.

Hata hivyo, magavana wamesisitiza kuwa hawatakubali kiwango chochote ambacho hakifiki Sh400 bilioni jinsi ilivyoidhinishwa na Seneti na Tume ya Ugavi wa Mapato.

Magavana wanasema mwanya wa fedha ambao upo kutokana na mapato ya serikali lazima ujazwe na serikali kuu jinsi ilivyowekwa kwenye Sheria ya Mwongozo wa Ugavi wa Mapato ya Kaunti (DoRA) 2024.“Tumeafikiana kukataa pendekezo la kupunguza mgao wa kaunti kwa Sh20 bilioni.

Hatua hii iwapo itatekelezwa na Wizara ya Fedha, itachangia kudorora kwa huduma katika kaunti na kurejesha nyuma mfumo wa utawala wa ugatuzi,” akasema Gavana wa Kakamega Farnandes Barasa.Aidha, alitilia shaka msingi wa sheria utakaotumiwa kukata Sh20 bilioni ambazo zinastahili kuelekezwa kwa kaunti.

Bw Barasa alikuwa akiongea katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega alipokagua shehena ya dawa za thamani ya Sh60 milioni ambazo zimenunuliwa na serikali ya kaunti.

Dawa hizo zilinunuliwa kutoka kwa Mamlaka ya Kusambaza Dawa na Vifaa vya Kimatibabu (KEMSA).

Gavana huyo alisema sekta ya Afya inakabiliwa na changamoto kadhaa katika ngazi ya kaunti huku wagonjwa wanaosaka huduma za kimatibabu wakiumia mno.“Wizara ya Fedha inastahili kuelewa mahitaji ya Wakenya na kupanga ili pesa hizo zitolewe kwa wakati kusaidia magavana kutimiza wajibu wao kwa raia. Pia, ni kupitia pesa hizi ambapo kaunti huwalipa wafanyakazi wao mishahara na kuimarisha huduma za afya,” akaongeza.

Magavana sasa wanataka mwongozo wa DoRA utumiwe badala ya Mwongozo wa Kutoa Mapato kwa Kaunti (CARA) ambao ni mswada na bado haujawasilishwa kwa seneti ili kaunti zipate pesa.

Wakati huo huo, magavana wamelitaka Bunge liharakishe mswada ambao ukipitishwa utaishurutisha serikali kuu kuchapisha ripoti ya kila mwezi kuhusu mgao ambao kila kaunti imepewa.

Mswada huo utahakikisha kuwa pesa zinatumwa kwa kaunti kwa kuzingatia idadi ya watu, viwango vya umaskini na miundomsingi.Mwongozo huu mpya unalenga kuhakikisha kuwa kaunti ambazo zina uchumi mdogo zinaimarika na kustawi kama zile zenye uwezo mkubwa wa mali.

Aidha, magavana wanadai kuwa kucheleweshwa mgao kumesababisha madeni wanayodaiwa na KEMSA yawe mengi na kufanya iwe vigumu kununua dawa kisha kuzifikisha kwa kaunti kwa wakati.

Bw Barasa alisema kuwa wamekuwa wakipata mgao baada ya miezi mitatu. Hatua hii imekuwa ikitatiza kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo kwa muda ambao uliwekwa.