Habari za Kitaifa

Wafanyakazi wa usafiri angani waahirisha mgomo

Na CHARLES WASONGA September 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SHUGHULI zitaendelea Jumatatu, Septemba 2, 2024 katika viwanja vya ndege nchini kama kawaida baada ya Chama cha Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi wa Usafiri Angani (KAWU) kuahirisha mgomo wao ulioratibiwa kuanza siku hiyo.

Kwenya taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Katibu Mkuu wa chama hicho Moses Ndiema alisema chama hicho kilichukua hatua hiyo baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja Vya Ndege (KAA) kuwapa stakabadhi za ukodishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Mamlaka hiyo inapanga kukodisha uwanja huo kwa Kampuni ya Adani Group kutoka India kwa muda wa miaka 30.

Bw Ndiema alisema uwasilishwaji wa stakabadhi hizo za mkataba wa ukodishaji ulikuwa moja kati ya matakwa ya chama cha KAWU.

“Tumejadili kuhusu suala hilo leo (Jumamosi) na tukaamua kwamba tucheleweshe mgomo wetu kwa siku saba. Hii ni baada ya usimamizi wa KAA kutimiza takwa letu la kwanza, kwa kutoa stakabadhi za ukodishaji wa JKIA kwa kampuni ya Adani,” Ndiema akasema.

Chama hicho kilitangaza nia ya kugoma kuanzia Jumatatu kulalamikia hatua ya serikali kuendesha mipango ya ukadishaji wa sehemu ya JKIA kwa kampuni ya Adani bila kuihusisha.

Aidha, KAWU ilidai serikali, kupitia KAA, inapania kukodisha uwanja bila kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa.

Sasa KAWU inasema inachambua kwa kina stakabadhi hizo za ukodishaji kwa lengo la kuhakikisha kuwa matakwa yao yanazingatiwa kabla ya kutoa mwelekeo kwa wanachama wake.

“Matokeo ya ukaguzi wake wa stakabadhi na mazungumzo yatakayofuata yatatumika kubaini ikiwa mgomo wetu utaendelea baada ya siku saba au la,” ikasema taarifa hiyo ya Bw Ndiema.

Uongozi wa chama hicho unakariri umuhimu wa mchakato huo wa ukodishaji kuendeshwa kwa njia ya uwazi na shirikishi, ikizingatiwa kuwa mpango huo unaweza kuathiri haki za wafanyakazi na mustakabali wa uwanja wa JKIA.

Wanachama wa KAWU wanahofu kwamba baadhi yao watapoteza kazi au mishahara yao kupunguzwa kampuni ya Adani ikichukua usimamizi wa JKIA.

Aidha, inakisiwa kuwa ada za huduma katika JKIA, zikiwemo nauli za ndege, zitapanda.