KUPPET: Mgomo wa walimu unaendelea
SHUGHULI za masomo zitaendelea kukwama katika zaidi ya shule 4,000 za upili za umma nchini kwa wiki ya pili kuanzia Jumatatu, Septemba 2, 2024.
Hii ni baada ya Chama cha kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) kushikilia kuwa mgomo wao utaendelea.
Akiongea na wanahabari Jumapili, Septemba 1, 2024 baada ya mkutano wa Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) ya chama hicho, Katibu Mkuu Akelo Misori alisema hitaji lao kuu la kupandishwa vyeo kwa walimu halijatimizwa.
“Hatupambani kwa sababu ya nyongeza ya mishahara ya kima cha Sh 1,000 pekee. Suala kuu ni kutopandishwa vyeo kwa walimu waliohitimu baada ya kuwekeza pesa nyingi kujiongeza masomo. Walimu wana mikopo ya kulipa kando na mahitaji mengine na ikiwa hawatapandishwa vyeo inavyohitajika hii ni sawa na kuhujumu juhudi zao,” akawaambia wanahabari baada ya mkutano huo uliofanyika katika Mkahawa wa Kasarani Sports View, Nairobi.
Kuppet imekuwa ikiitaka Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kuwapandisha vyeo walimu zaidi ya 130,000 ambao walishiriki na kupita mijarabu ya kupandishwa vyeo mwaka wa 2024.
Wiki jana, Serikali ilitoa Sh13.7 bilioni za kufadhili awamu ya pili ya nyongeza ya mishahara ya walimu kulingana na Mkataba wa Makubaliano (CBA) ya 2021-2025.
Ni nyongeza hiyo ndiyo Kuppet inataja kama “suala lisilo na uzito zaidi” miongoni mwa yale yaliyoichangia kuitisha mgomo wa wanachama wake kuanzia Agosti 26, 2024.
Bw Akelo pia aliitaka serikali kupitia TSC kuwapa ajira ya kudumu, walimu 46,000 vibarua wanaofundisha katika Shule za Upili za Msingi (JSS).
“TSC inafaa kuwaajiri walimu 46,000 ambao wanataka kujiunga na Kuppet. Hamna haja kwa tume hiyo kuwatumia wataalamu hawa vibarua ilhali wamehitimu vya kutosha sawa na wenzao,” akaeleza.
Mnamo Jumatano wiki jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia aliwaagiza walimu hao wa JSS kujaza fomu hitajika ili kuongeza kandarasi yao kwa miezi minne zaidi. Kandarasi hiyo ilitarajiwa kukamilika Agosti 30, 2024.
TSC inaongeza muda wa kandarasi ya walimu hao wakati ambapo serikali imekuwa ikishikilia kuwa imetenga Sh18.5 bilioni za kufadhili mpango wa kuwapa ajira ya kudumu.
Wiki iliyopita Waziri wa Fedha John Mbadi alitoa hakikisho kuwa pesa hizo zipo.
Waziri huyo alisema hayo siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Ndindi Nyoro kushikilia kuwa pesa hizo (Sh18.5 bilioni) ziko “salama” na haziwezi kuelekezwa kwa matumizi mengine.