Biashara bandari ya Kisumu yanoga
BANDARI ya Kisumu ambayo ilikarabatiwa kwa kima cha Sh3 bilioni inaendelea kufanya vizuri baada ya kuongezeka kwa mizigo inayosafirishwa na vyombo vya usafiri hadi mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa takwimu ya Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA), bandari hiyo inatarajiwa kupita kiwango cha zaidi ya tani 200,000 ya mizigo inayosafirishwa kila mwaka.
Takwimu hizo ambazo ni matokeo ya nusu ya 2024, zilionyesha kuwa idadi ya tani ya mizigo ilipanda hadi 125,503 kutoka tani 60,910 nusu ya mwaka jana, 2023.
Pia, idadi ya vyombo vinavyosafirisha mizigo iliongezeka hadi 116 mwaka huu, 2024, kutoka 63 ikilinganishwa na mwaka jana, 2023.
“Kati ya vyombo ambavyo kwa sasa hutua katika bandari hiyo ni MV Uhuru ambayo imebebea vipuri vya tani 804.5 na inaelekea Uganda,” KPA ikasema kwenye ripoti yake.
Vilevile, inatarajiwa kuwa MV Uhuru II ambayo itazinduliwa hivi karibuni itafungua Ziwa Viktoria kwa uchukuzi wa majini kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.
Meli hiyo ambayo imejengwa Kenya ina uwezo wa kubeba tani 1,800 na itakuwa inabeba petroli na mizigo mingine.
Isitoshe, meli hiyo ina injini ya kisasa ambayo inaiwezesha kuenda kwa kasi ya juu.
Kutokana na hitaji ya petroli kwenye mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki, meli ya Uganda inayofahamika kama MT Kabaka Mutebi III pia itakuwa kati ya vyombo vya majini ambavyo vitakuwa vikitoka Kisumu kuelekea bandari za Port Bell na Jinja.
Usafiri katika miji hiyo imefufua kumbukumbu za 1901 enzi za Wakoloni ambapo bidhaa zilikuwa zikisafirishwa kupitia meli.
Kando na Uganda, uchukuzi kupitia Ziwa Viktoria umeimarisha shughuli kati ya Kenya na Sudan Kusini, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Kuimarishwa kwa shughuli kunaonyesha kuwa Kenya inapiga hatua na sasa tunalenga kutoa huduma za hadhi,” akasema Meneja Mkurugenzi wa KPA William Ruto.