KUPPET ilivyofanikiwa kutia TSC boksi na kusitisha mgomo
CHAMA cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET) kimefutilia mbali mgomo wa walimu wanachama wake, baada ya kuafikia maelewano na Tume ya Huduma za Walimu (TSC).
Muafaka huo umejiri baada ya baadhi ya walimu wa shule za upili kuagiza wanafunzi kurejea nyumbani kwa kukosa walimu wa kuwafundisha.
Wakiongea na wanahabari Jumatatu, Septemba 2, 2024 baada ya mkutano wa saa kadhaa katika makao makuu ya TSC, Nairobi maafisa wa tume hiyo na viongozi wa KUPPET walisema wamekubaliana kuhusu “masuala muhimu” yaliyosababisha mgomo huo.
“Kutoka upande wetu, tumesitisha mgomo na kuwataka walimu wetu wote kurejea madarasani kusubiri kusuluhishwa kwa masuala haya kulingana na makubalianao kati yetu na tume,” akasema Katibu Mkuu wa KUPPET Akelo Misori.
Katibu huyo alisema KUPPET itatoa maelezo zaidi baadaye kwa misingi ya matokeo ya uamuzi wa mahakama unaotarajiwa kutolewa Alhamisi.
Nayo TSC imeahidi kutowaadhibu walimu wa shule za upili walioshiriki mgomo huo ulioanza Jumatatu, Agosti 26, 2024.
“Tumekubaliana kuhusu mpango wa kurejea kazini na hamna atakayeadhibiwa kwa njia yoyote ile kwa kushitiki mgomo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia.
Naye Bw Misori alisema malalamishi yao kuhusu bima ya afya yameshughulikiwa na fedha za kuifadhili kurejeshwa katika bajeti.
“Kuhusu suala la kupandishwa vyeo kwa walimu, tovuti ya kuifanikisha imefunguliwa na TSC na imeanza kusaka fedha za kufadhili mpango huo. Masilahi ya walimu wakuu na manaibu walimu wakuu ambao wamekuwa wakihudumu kama kaimu pia yatashughulikiwa,” Bw Misori akasema.
Dkt Macharia alisema kuwa TSC imetoa Sh13.7 bilioni za kufadhili makubaliano kuhusu nyongeza ya mishahara ya walimu (CBA) ya 2021-2025.
“Malipo hayo yametolewa ambapo walimu wamelipwa malimbikizi ya kuanzia Julai 1, mwaka huu, 2024” akaeleza.
Awali, zaidi ya shule 100 za upili za umma ziliwatuma nyumbani wanafunzi kutokana na hofu ya kutokea kwa fujo na uharibifu wa mali wakati wa mgomo.