Arati anavyoumishwa kichwa na wahudumu wa afya mgomo ukinukia
WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Kisii wametishia kususia kazi wakilalamikia hatua ya serikali ya gatuzi hilo kuchelewa kuwapandisha vyeo na masuala mengine yanayohusu bima yao ya matibabu.
Maafisa wa Muungano wa Wauguzi nchini (KNUN), Muungano wa Maafisa wa Kitabibu (KUCO), na Muungano wa Madaktari Nchini (KMPDU), wamesema utawala wa Gavana Simba Arati umekataa waziwazi kuheshimu makubaliano ya kurejea kazini yaliyotiwa saini kati yao na serikali miezi minne iliyopita, walipokuwa mgomoni.
Wakihutubia wanahabari mnamo Jumanne, Septemba 3, 2024 mjini Kisii, maafisa hao walisema mnamo Mei 8, 2024, madaktari walikubali kusitisha mgomo wao wa kitaifa ambao ulikuwa umedumu kwa siku 56 baada ya mahakama kuwaagiza kutia sahihi mbinu ya kurejea kazini na serikali.
Stakabadhi za makubaliano hayo ziliwasilishwa kortini na ikakubaliwa kuwa kaunti zote zinapaswa kuwapandisha vyeo madaktari wote ambao walipaswa kupandishwa vyeo na kuwa na bima ya matibabu iliyoimarishwa kufikia Septemba 1, 2024.
Lakini kulingana na Dkt Aggrey Orwenyo, Katibu Mkuu wa KMPDU tawi la Nyanza, Serikali ya Kaunti ya Kisii haijaonyesha juhudi zozote za kuwapandisha vyeo wanachama wao na hivyo kutangaza kwamba watasusia kazi tena baada ya wiki mbili ikiwa hakutakuwa na mabadiliko.
Dkt Orwenyo aliripoti kuwa uongozi wa kaunti zote za Nyanza ulionyesha nia njema katika kushughulikia malalamishi ya wahudumu wa afya isipokuwa Kisii, ambayo alidai viongozi wake walikuwa wakiwahadaa.
“Hatujapata dalili zozote za kaunti (Kisii) kuwa tayari kushughulikia masuala yote ambayo yaliwafanya madaktari kugoma. Ninaweza kuripoti kwamba hapa Nyanza, kamati za Makubaliano ya Pamoja (CBA) katika kaunti zote tano zimekutana isipokuwa Kisii. Tumeomba uongozi wa kaunti kuitisha mikutano kamili ili tuangazie masuala yanayoathiri madaktari wetu lakini hatujawahi kuwa nayo,” Dkt Orwenyo alisema.
“Kwa sababu ya hayo, tumeamua kuwa baada ya wiki mbili, tutaanza mgomo wetu ambao hujawahi kushuhudiwa. Ni barua za kupandishwa vyeo zitaturudisha kazini,” Katibu Mkuu wa KNUN Kisii Moses Riang’a aliongeza.
Taifa Dijitali ilijaribu kuwasiliana na Waziri wa Afya wa Kisii Ronald Nyakweba ili atoe maoni yake kuhusu masuala yaliyoibuliwa na vyama vya wahudumu hao, lakini msimamizi huyo hakujibu simu wala arafa zetu kufikia kuchapishwa kwa taarifa hii.