Habari za Kitaifa

Mkenya akana madai ya kumuua mpenziwe Amerika

Na RICHARD MUNGUTI September 4th, 2024 3 min read

MKENYA Kevin Kang’ethe alishtakiwa Jumanne, Septemba 3, 2024 nchini Amerika kwa madai ya mauaji ya mpenziwe, Margaret Mbitu.

Kang’ethe aliyetorokea Kenya Novemba 2023 baada ya kushukiwa kumuua Mbitu, alikana kumuangamiza mpenziwe Oktoba 31, 2023.

Alishtakiwa katika Mahakama Kuu ya Suffolk, Boston Amerika.

Alizuiliwa gerezani hadi Novemba 5, 2024 kesi hiyo itakapoanza kusikizwa.

Keng’ethe alisafirishwa kutoka gereza la Viwandani Septemba 1, 2024 baada ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi, Lucas Onyina kuruhusu ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Kenya (DPP) Renson Ingonga, kwamba arudishwe Amerika kushtakiwa kwa mauaji ya Margaret Mbitu.

“Keng’ethe alisafirishwa kutoka gereza la Viwandani Septemba 1, 2024 hadi Amerika. Alifika Boston Septemba 2, 2024 kushtakiwa kwa mauaji ya Margaret Mbuitu,katika Mahakama kuu ya Suffolk iliyoko Pemberton Square, jimbo la Boston,” Bw Ingonga alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu, Septemba 2, 2024.

Bw Ingonga alihihakikishia serikali ya Amerika ataipa msaada wowote inayotaka wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili Kang’ethe.

Wakati wa mashauri na mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai wa Amerika Bw Christopher Wray Jijini Nairobi mnamo June 2024, Ingonga alimhakikishia kwamba Kang’ethe atarudishwa Amerika kushtakiwa kwa mauaji ya Margaret Mbitu.

Baada ya kumuua mpenziwe miezi miezi 10 iliyopita, Keng’ethe aliufungia mwili wa Mbitu ndani ya gari lake na kuliegesha ndani ya gareji iliyoko Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Logan, alipokuwa akifanya kazi ya uhandisi wa ndege.

Kang’ethe aliyekwepa mkono mrefu wa sheria, alikuwa amejificha katika eneo la Parklands Nairobi makachero walipomtia nguvuni.

Picha yake ilikuwa imesambazwa na polisi wa kimataifa kwamba “ni mtu anayesakwa kwa kushtakiwa kwa tuhuma za mauaji USA.”

Alikamatwa Januari 30, 2024 na maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) waliokuwa wakimsaka kwa udi na uvumba baada ya kuamriwa na serikali akamatwe.

Serikali ya Amerika kupitia Wizara ya Mashauri ya Kigeni ilikabidhi afisi ya Mwanasheria Mkuu uchunguzi wa mauaji ya Mbitu na shtaka la mauaji atakaloshtakiwa Kang’ethe.

Amerika iliomba mshukiwa arudishwe nchini humo kujibu mashtaka kwa mujibu wa sheria za jimbo la Massachusetts, ndizo General Law.

Bw Igonga, kupitia kwa wakili wa serikali Vincent Monda aliwasilisha ombi la Amerika na kumsihi Onyina aruhusu mshukiwa apelekwe nchini humo kukumbana na makali ya sheria.

Baada ya kutathmini ushahidi wote aliowasilisha DPP kupitia kwa Bw Monda, hakimu alifikia uamuzi kwamba kuna ushahidi wa kutosha Kang’ethe kufunguliwa mashtaka ya mauaji dhidi ya Mbitu Amerika.

Bw Onyina alisema DPP aliwasilisha ushahidi wa kutosha kwamba Kang’ethe alihusika na mauaji ya mpenzi wake.

“Baada ya kuchambua ushahidi wote uliowasilishwa na DPP hii mahakama imebaini kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuwezesha Kang’ethe kufunguliwa shtaka la mauaji nchini Amerika,” Bw Onyina aliamua.

Mahakama ilisema sheria za Kenya na za Amerika kuhusu kesi za mauaji zinawiana.

Korti ilisema Kang’ethe alikuwa na uhusiano na Mbitu na kwamba alihusika na mauaji yake kabla ya kutorokea Kenya.

“Kutokana na ushahidi uliowasilishwa kutoka Amerika ni bayana sheria za kesi za mauaji zinalingana na hakuna tashwishi kosa la mauaji lipo kwenye sheria za nchi hii ya ng’ambo jinsi ilivyo hapa nchini Kenya,” Bw Onyina alisema katika uamuzi wake.

Hakimu alisema Kang’ethe harudishwi Amerika kwa sababu za kisiasa, bali kukabiliwa na makali ya sheria kwa madai ya kuua Margaret Mbitu.

Hakimu alisema kwa mujibu wa sehemu ya 5 ya Sheria za Uhalifu Kifungu nambari 63, mahakama imepewa mamlaka kuamuru mshukiwa asafirishwe kujibu shtaka ng’ambo ikiwa kuna ushahidi wa kutosha.

Kang’ethe alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri alipokamatwa kuhusiana na mauaji ya Mbitu katika eneo la Lowell, jimbo la Massachusetts Oktoba 31, 2023 Amerika.

Bi Mbitu alikuwa akitoa huduma za afya mjini Halifax jimbo la Massachusetts kabla ya kutoweka Oktoba 23, 2023.

Juhudi za kumsaka Mbitu hazikufua dafu.

Familia yake ilitoa habari za kutoweka kwake katika kituo cha Polisi cha Whitman.

Habari zilienea kuhusu kupotea kwake kupitia polisi wa jimbo la Massachusetts.

Uchunguzi ulibaini Mbitu alitoka kazini akiandamana na Kang’ethe aliyekuwa akiendesha gari jeupe, muundo wa Toyota Venza

Polisi walibaini kuwa Kangethe alimshambulia Mbitu kwa kumdungadunga kwa kisu na kumuua.

Hatimaye, alifunika mwili wa mpenziwe kwa chandarua ndani ya gari lake aliloacha ameegesha katika gareji katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Logan (Logan

Novemba 1, 2023 polisi waliupata mwili wa Mbitu ukiwa umeketishwa katika kiti cha mbele cha gari la Kang’ethe.

Alitorokea Kenya kupitia uwanja wa ndege wa JKIA na kujificha katika kijiji cha Gachie, Kiambu.

Mahakama ilisema Kang’ethe alikuwa anatumia simu za marafiki kuwasiliana na marafiki zake jijini Nairobi na Amerika.

Mahakama ilitupilia mbali ushahidi wa Kang’ethe kwamba hakuhusika kwenye mauaji ya mpenziwe.

[email protected]