SHIRIKA la ndege la Kenya Airways limewaomba radhi wateja wake kutokana na hitilafu za hivi majuzi iliyosababisha baadhi ya safari kucheleweshwa. 
Katika taarifa ya Jumatano, Septemba 4, shirika hilo lilisema kuwa tatizo hilo lilisababishwa na hitilafu za injini ambayo haikutarajiwa.
“Kenya Airways ingependa kuomba radhi kwa ucheleweshaji na usumbufu ambao umeshuhudiwa katika siku za hivi majuzi,” ilisoma sehemu ya taarifa kutoka kwa Kampuni ya Mawasiliano ya shirika hilo.
Kenya Airways iliongeza, “Haya yamesababishwa na hitilafu ya injini na vikwazo visivyotarajiwa; hivyo kusababisha tusitishe safari za ndege mbili (2)787 Dreamliner.”
Zaidi ya hayo, shirika la ndege la Kenya Airways lilisema kuwa lilikuwa likifanya kazi na kampuni inayolisambazia injini na watengenezaji wake kutafuta suluhu ya kudumu ya suala hilo.
Sehemu ya marekebisho, kulingana na shirika hilo la ndege ni kununua injini mpya.