PETER TABICHI: Mwalimu anayewapa matumaini wanafunzi kutoka familia maskini
Na MAGDALENE WANJA
SHULE ya Upili ya Keriko iko katika kijiji cha Pwani ambapo ni katika maeneo ya kipato cha chini ya Kaunti ya Nakuru.
Safari kuelekea katika eneo hilo ina changamoto tele kutokana na hali mbovu ya barabara na jua kali linalochoma.
Idadi kubwa ya wakazi wanatumia pikipiki kwa uchukuzi na magari machache tu yanaonekana barabarani.
Hata hivyo, shule hiyo iko katika mazingara matulivu kutokana na kivuli ambacho kinaipa kivuli kizuri.
Hiki ndicho kimekuwa kituo cha kazi cha mwalimu Peter Mokaya Tabichi kuanzia mwaka 2015 ambako amekuwa akifunza.
Bw Tabichi pia ni ndugu wa kikatoliki (Franciscan brother of the Catholic Church) na wanafunzi pamoja na walimu wana mazoea ya kumuita “Brother Tabichi”.
Tulipotembea shuleni humo, tulimpata Bw Tabichi na baadhi ya wanafunzi wakiwemo wawili wamekuwa wakienda shuleni wakati wa likizo kwa matayarisho ya shindano kuu la INTEL International Science and Engineering Fair 2019 ambalo litafanyika katika jimbo la Arizona, Amerika.
Tangu kujiunga na shule hiyo Bw Tabichi amebadilisha shule hiyo na kuifanya kituo cha kuwapa matumaini wanafunzi kutoka familia duni ambao wengi hawana uwezo wa kujikimu kimaisha.
Bw Tabichi alifunza katika shule ya kibinafsi katika kaunti ya Nakuru baada ya kufuzu kutoka chuo kikuu cha Egerton Mnamo mwaka 2009.
Shule hiyo iliyomilikiwa na kanisa la Katoliki ilikuwa na vifaa muhimu ambavyo viliwawezesha wanafunzi kusoma bila matatizo yoyote.
Hii ilikuwa hadi mwaka 2015 ambapo aliona tangazo la nafasi za kazi katika kaunti ya Nakuru lilowekwa na tume ya kuwaajiri walimu ya TSC.
Alipoomba nafasi ile, alibahatika kuwa mmoja wa waliofuzu kupata nafasi za kazi.
Alipata barua ya kumuarifu kuwa alitarajiwa kufanya kazi katika shule ya upili ya Keriko, nafasi ambayo aliichukua bila kusita.
“Nilipofika katika shule hiyo, hali ilikuwa tofauti na hali ya umaskini ilikuwa ya kutisha,” alisema Bw Tabichi.
Eneo la shule hiyo lilikuwa na matatizo mengi yakiwemo changamoto za mawasiliano haswa kutumia simu ya mkononi.
“Shule hiyo ilikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walitoka katika familia maskini sana, baadhi yao walifika shuleni kama hawajapata kiamsha kinywa na walisinzia darasani,” akasema Bw Tabichi.
Kutokana na hali hii, aliamua kuanza safari ya kubadilisha maisha y a wanafunzi na wakazi wa eneo hilo ambao walikosa tumaini.
Alifanya mchango kutoka kwa baadhi ya marafiki zake ambapo aliweza kupata Sh 500,000, hela ambazo alizitumia katika kununua vifaa vya maabara.
“Kulikuwa na maabara moja pekee shuleni ambayo ilitumika na wanafunzi wote.Huu ndio ulikuwa mradi wa kwanza,”akasema Bw Tabichi.
Bw Tabichi pia aliunda klabu ya wanafunzi wenye talanta ambapo aliwapa nafasi ya kuendeleza vipaji mbai na masoma darasani.
“Pia niliweza kuwaleta wanafunzi pamoja kupitia klabu ya amani kwani wanafunzi katika shule hiyo wamezaliwa katika jamii tofauti,” aliongeza Bw Tabichi.
Hizi ni baadhi ya njia Bw Tabichi alitumia kubadilisha mawazo ya wanafunzi na wazazi wao kwa kuwapa tumaini.
Jambo hili lilichangia pakubwa katika matokeo ya mtihani ambapo wengi walianza kupata alama za juu ikilinganishwa na hapo hawali.
“Mnamo mwaka 2017, tuliweza kujiunga na mashindano ya Kenya National Science and Engineering Fair ambapo mojawapo ya miradi tuliyowasilisha ilikuwa njia bunifu ya kutoa nguvu za umeme kutokana na mimea,” alisema Bw Tabichi.
Mradi mwingine uliowasilishwa na wanafunzi wake ni ule wa kifaa cha Essameter ambacho nia yake ni kuwasaidia vipofu na viziwi kupima urefu.
Japokuwa kifaa hicho hakikufikia malengo ya shindano hilo, wanafunzi hao walikifanyia ukarabati ambao ulikifanya kushinda katika mashindano yam waka 2018.
Bidii yao iliifanya shule hiyo kuchukua nafasi ya pili nchini katika mashindano hayo ambayo ni ya 56 tangu kuanzishwa kwake.
Wanafunzi hao wawili wanatarajiwa kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya INTEL International Science and Engineering Fair ya mwaka 2019 nchini Arizona.
Mnamo mwezi Julai 2018, aliarifiwa na rafiki yake kwamba kuna mshindano ya kitaifa la Varkey Foundation Global Teacher Prize 2019.
“Sikutiia maanani ila nilijisajili na kutuma stakabadhi zilizoihitajika. Kwa kuwa nilikuwa nimepuuza swala hilo, nilijisajili siku ya mwisho ya shindano hilo,” anasema.
Mnamo mwezi Novemba, Bw Tabichi alipokea barua pepe ya kumjulisha kwamba alikuwa baadhi ya walimu 50 duniani waliochaguliwa katika shindano hilo.
“Sikuamini habari hiyo na nilikaa usiku kucha bila kupata lepe la usingizi ,” akasema Bw Tabichi.
Shindano hio lilikuwa limewavutia washiriki 10,000 kutoka nchi 179 duniani.
Baadhi ya mambo ambayo Bw Tabichi ameyafanya na kuwawacha walimu wenzake vinywa wazi ni kwamba anapokea asilimia 20 pekee ya mshahara wake na idadi inayosalia, anaitoa kuwasaidia wasiojiweza.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw Daniel Mwariri, ijapokuwa Bw Tabichi amesaidia pakubwa katika mabadiliko shuleni humo, shule hiyo bado ina mahitaji mengi.
“Tuna kompyuta moja pekee ambayo hutumika na karani na kila kitu kinachohitaji kuchapishwa, tunatumia mashine hiyo,” alisema Bw Mwariri.
Bw Mwariri aliongeza kuwa kutongana na hali ngumu na kiangazi katika eneo hilo, baadhi ya walimu huacha kazi baada ya muhula mmoja, jambo lililochangia pakubwa katika upungufu wa walimu.
Licha ya changamoto hizo, shule hiyo imeweza kusalia katika orodha ya shule bora katika kaunti ya Nakuru.