Habari za KitaifaMakala

Ujio wa Raila ulivyopiga breki UDA kumeza ANC

Na CHARLES WASONGA September 8th, 2024 2 min read

KASI ya mpango wa Amani National Congress (ANC) kujiunga na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) sasa inaonekana kupungua baada ya viongozi wa ODM kutangaza nia ya kushirikiana na Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Duru katika ANC zimeiambia Taifa Leo kwamba baada ya Rais kuwashirikisha viongozi wa ODM katika serikali yake kwa kuwateua mawaziri, lengo la kufikiwa kwa umoja wa kitaifa sasa linaelekea kutimizwa.

“ANC na UDA zilipania kuungana kwa lengo la kuleta uthabiti ndani ya muungano wa Kenya Kwanza na kupalilia umoja wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Lakini kwa kuwa wenzetu wa ODM wamekubali kujiunga nasi serikalini na Rais akateua watano kati yao kuwa mawaziri, hatuna dharura ya kuungana na UDA kwa sababu serikali iliyoko sasa ni thabiti na shirikishi,” akasema mbunge mmoja ANC aliyeomba tulibane jina lake.

Baada ya Rais Ruto kupata mapokezi mazuri katika ziara ya siku nne eneo la Nyanza, wandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga wameahidi kushirikiana na Rais Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, Seneta wa Siaya Oburu Oginga miongoni mwa wengine wanashikilia kuwa hamna kitakachowazuia kufanyakazi na Dkt Ruto ikiwa atatimiza ahadi kadhaa alizotoa juzi kwa wakazi wa eneo hilo.

“Rais Ruto amerudisha mkono kwa vitendo baada ya Baba (Raila) kumsaidia kuleta utulivu serikalini. Ameonyesha hilo kwa kuteua wenzetu watano katika baraza la mawaziri. Kwa hivyo, hatutamwacha bali tutasimama naye mpaka 2027,” anasema Mbunge huyo wa Suna Mashariki.

Kwa upande wake Dkt Oginga, ambaye ni kaka mkubwa wa Bw Odinga, anasema wakazi wa Nyanza wanatambua kuwa mnamo 2007 Dkt Ruto alimsaidia Odinga kuwa Waziri Mkuu na hivyo wako tayari “kurudisha mkono”.

“Kwa hivyo, tunafurahi kuwa Rais ameteua wanachama watano wa ODM kuwa mawaziri katika serikali yake na tunataraji kwamba atawateua wengine katika nyadhifa zingine. Huyu ni rafiki wa dhati ambaye tutamuunga mkono hadi mwisho,” anaeleza.

Walioteuliwa juzi katika baraza la mawaziri ni waliokuwa manaibu wa kiongozi wa chama hicho, Bw Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa mwenyekiti John Mbadi, aliyekuwa kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi na aliyekuwa mwanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uchaguzi katika ODM Beatrice Askul Moe.

Bw Joho ni Waziri wa Uchumi wa Majini na Uchimbaji Madini huku Bw Oparanya akiongoza wizara ya Ustawi wa Vyama vya Ushirika.

Naye Bw Mbadi ni Waziri wa Fedha huku Wandayi akihudumu kama Waziri wa Kawi na Bi Askul akisimamia Wizara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

Bw Martin Andati ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuwa baada ya ODM “kuingia serikalini” bila shaka mchakato wa kuunganisha vyama vya ANC na UDA utakufa.

“Japo ANC ilisema haja yake ya kuungana na UDA ilikuwa ni kuleta umoja nchini, haja kuu ilikuwa ni kukabiliana na uasi kutoka kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na wandani wake. Kwa hivyo, sasa ambapo Raila na watu wake wamekubali kujiunga serikali, uasi huo umeyeyushwa bila shaka hamna haraka ya kuviunganisha vyama hivyo viwili,” anaeleza.

Mnamo Juni 19, mwaka huu, vyama vya ANC na UDA vilitangaza nia ya kuungana na kuwa chama kikubwa chenye nguvu zaidi.

Tangazo hilo lilitolewa kufuatia mkutano wa viongozi wakuu wa vyama hivyo, uliofanywa katika Ikulu ya Nairobi na kuongozwa na kiongozi wa UDA Rais Ruto na kiongozi wa ANC Gavana wa Lamu, Issa Timamy.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye ndiye mwanzilishi wa ANC pia alihudhuria.