Habari za KitaifaMakala

Joto kambi ya Raila na Ruto endapo vyama vya UDA na ODM vitaungana kuelekea 2027

Na MOSES NYAMORI September 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WANDANI wa Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga ambao wanamezea mate nyadhifa mbalimbali 2027 wameanza kuingiwa na kiwewe kuhusu hatima yao iwapo vyama vya UDA na ODM vitakuwa na muungano wa kisiasa.

Hatua ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kusalia katika mrengo wa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ni ishara tosha kuibuka kwa kiwewe hicho.

Bw Owino ametangaza kuwa atawania ugavana wa Nairobi dhidi ya gavana wa sasa Johnson Sakaja, na anahofia huenda muungano wa UDA na ODM utagawa viti Nairobi na kumfungia nje ya Ugavana.

Taifa Leo imebaini kuwa wanasiasa kwenye mirengo ya Rais na Bw Ruto kwenye kaunti za Mombasa, Kisii, Kakamega na Homa Bay wameanza kutathmini nafasi yao hasa wale ambao walikuwa wakilenga kuwapinga magavana wa sasa.

Hali ni hiyo hiyo kwenye maeneo ambayo vyama vya ODM na UDA  vina uungwaji mkono mkubwa.

Kisii

Katika Kaunti ya Kisii, Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro ambaye ni hasimu mkubwa wa Gavana Simba Arati naye ametangaza kuwa analenga kiti cha ugavana mnamo 2027.

Wanasiasa kwenye mirengo yote miwili wanahofia kuwa kutakuwa na maelewano au muafaka kati ya ODM na UDA ili kuzuia wawaniaji wa vyama hivyo viwili kumenyania viti vya kisiasa hasa ugavana.

Katika uchaguzi wa 2022 kulikuwa na baadhi ya wanasiasa ambao walizuiwa kuwania baadhi ya viti kutokana na maelewano yaliyokuwa kati ya vyama tanzu ndani ya Azimio na pia vyama vilivyokuwa katika Kenya Kwanza.

Mombasa

Katika Kaunti ya Mombasa, Mbunge wa Nyali Mohamed Ali anaonekana kutochangamkia ushirikiano wa UDA na ODM.

Hii ni kwa sababu duru zinaarifu analenga ugavana ambao unashikiliwa na Abdulswamad Nassir ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM.

“Hata kama nimekumbatia serikali jumuishi, nataka kuwahakikishia wakazi wa Mombasa kuwa kilio chao cha uongozi bora na uwajibikaji bado nitakipigania,

“Wakazi wa Mombasa wameteseka sana kwa sababu utawala wa kaunti haujafanya maendeleo yoyote tangu uingie mamlakani miaka miwili iliyopita. Hawajajenga hata choo kuhakikisha usafi,” akasema Bw Ali.

Wakati wa ziara yake Nyanza, Rais Ruto aliwaambia wakazi kuwa yupo tayari kushirikiana na Bw Odinga kwenye uchaguzi wa 2027.

Mwaka huo Rais naye atakuwa akisaka uungwaji mkono ili kupata awamu ya pili.

Ili kujihakikishia uungwaji mkono wa ODM Nyanza, huenda ikaamuliwa kuwa UDA haitawasimamisha wagombea eneo hilo, Magharibi na Pwani ambako chama hicho kinajivunia uungwaji mkono mkubwa.

Wale ambao wanamezea mate viti vya ugavana ndio huenda wakaathiriwa.

Kwa sasa magavana wa ODM Pwani, Magharibi na Nyanza ambao wanahudumu muhula wao wa kwanza na watakuwa wakisaka wachaguliwe tena ni  Arati (Kisii), Fernandes Barasa (Kakamega), Nassir (Mombasa) naPaul Otuoma (Busia).

Katika Kaunti ya Homa Bay, Gavana wa zamani wa Nairobi Evans Kidero analenga kiti cha Bi Wanga kupitia UDA.

Bw Sakaja naye alisema kuwa kwa sasa jambo la muhimu ni kuwaleta Wakenya pamoja na hilo halifai kuyumbishwa na siasa za 2027.

“Ni mapema sana kusema huyu ama yule atanufaika au kupoteza iwapo ODM itaanza ushirikiano na UDA. Binafsi siogopi ushindani wa kisiasa na sitaki niidhinishwe,” akasema Bw Sakaja.

“Nimekuwa nikuhubiri umoja hata tangu enzi za Uhuru Kenyatta. Tuunge mkono umoja wetu na wakati ukija tushindane kwa haki,” akaongeza.

Licha kuchaguliwa kupitia UDA, wabunge na madiwani wa ODM ndio wamekuwa watetezi wakubwa wa Bw Sakaja. Bw Owino ndiyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Bw Sakaja ndiposa ameamua kusalia na Bw Musyoka hata baada ya viongozi wengi wa ODM kuanza kushabikia serikali.

“Mimi ni mwanachama wa ODM na nitaendelea kutia mizani serikali. Hakuna ubaya wa kusalia na Kalonzo kwa sababu sote tuko Azimio na ODM iko kwenye muungano huo,” akasema Bw Owino ambaye analenga kiongozi wa ODM baada ya Raila kuelekeza macho yake kwenye uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Katika Kaunti ya Kakamega Seneta Boni Khalwale pia atajipata pabaya kutokana na ushirikiano wa UDA na ODM kwa kuwa amekuwa akipanga kumpinga Bw Barasa.

Bw Khalwale anaonekana kuungwa mkono na Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogondogo Wycliffe Oparanya ambaye amekosana na Bw Barasa.

Seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malala ambaye aliwania ugavana kupitia UDA mnamo 2022 naye amekosana na Rais Ruto na aliondolewa kama katibu mkuu wa chama hicho.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo