Habari za Kitaifa

Sababu ya viongozi wa wanafunzi vyuoni kuahirisha maandamano kupinga mfumo wa ufadhili

Na MERCY SIMIYU, KEVIN CHERUIYOT   September 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wamesitisha maandamano yaliyofaa kuanza Jumatatu Septemba 9, 2024 na kuipa serikali  makataa ya siku 30 kushughulikia masuala mbalimbali yanayoathiri elimu vyuoni.

Wanafunzi hao wamekuwa wakilalamikia mfumo mpya wa ufadhili ambao wanasema unabagua na kufasiri elimu ya chuo kikuu kama ya matajiri pekee.

Hatua yao ilijiri huku Wizara ya Elimu ikilegeza kamba kutokana na shinikizo za wanafunzi kuhusu mfumo huo.

Wizara imetangaza kuwa mfumo huo utafanyiwa marekebisho ili wanafunzi kutoka familia maskini wasifungiwe nje au kupewa mgao mdogo jinsi ilivyo kwa sasa.

Kupitia taarifa, wizara ilisema kuwa imebuni kamati mbili ambazo zinawashirikisha viongozi wa wanafunzi, wataalamu, washikadau ambao wataangazia upya mfumo huo.

“Hii itahakikisha kuwa wanafunzi wameshirikishwa katika kuafikia marekebisho kwenye mfumo huo,” ikasema taarifa kutoka wizara.

Katika kikao cha Jumapili, viongozi wa wanafunzi walitambua juhudi za serikali hasa pendekezo la wizara ya elimu kukumbatia mfumo ambao utaongeza mgao kwa kila mwanafunzi.

Hii itawasaidia kupambana na gharama ya juu ya maisha nchini kwa kupata mahitaji ya kimsingi wakiwa vyuoni.

“Kama viongozi, tunatambua juhudi za wizara na serikali kuibuka na marekebisho ya kuamua mfumo mpya wa ufadhili ambao unawanufaisha wanafunzi katika kila tapo.

“Kuwahusisha wanafunzi kwenye jopo hilo ni hatua nzuri hasa ikilenga kuwaokoa wanafunzi kutoka kwa gharama ya juu ya maisha,” akasema Zadock Okoth, Kiongozi wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Viongozi hao walikashifu serikali kwa kuwapuuza wakati wa kuibuka na mfumo wa ufadhili ambao walisema ulikuwa na ubaguzi na hawatasita kuupinga iwapo utaendelea kutekelezwa.

“Mazungumzo ni lugha ambayo serikali imekuwa ikitumia kutupumbaza. Serikali imekuwa ikitoa ufafanuzi kuhusu mfumo huo ilhali haikusaka maoni ya wanafunzi au wawakilishi wao kabla ya kuutekeleza,” akaongeza Bw Okoth.

Gharama ya juu ya makazi na  mwongozo wa kulipa karo ambao si nafuu kwa wazazi ni kati ya masuala ambayo pia wanataka yaangaziwe. Wanafunzi wanasisitiza kuwa mabadiliko kwenye mfumo wa sasa utafanya elimu iwe gharama nafuu kwa wanafunzi kutoka familia maskini.

Kuhusu kuzima maandamano yao, wanafunzi hao walisema walipata habari kuwa kuna baadhi ya maafisa wa usalama ambao walipanga kujifanya wanashiriki kisha kuwadhuru wanafunzi.

“Tumegundua kuwa kulikuwa na mpango wa kuwaingiza polisi kati yetu wakati wa maandamano yao. Kwa kuzingatia usalama wa wanafunzi, tunaamini kuwa kwa wakati huu tusielekee njia hiyo ya maandamano,” akaongeza Bw Okoth.

Katibu Mkuu wa uongozi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Nairobi  Ramex Saxena, Kiongozi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Chuka Adrian Oluoch na Clare Gathoka kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta walihudhuria kikao na wanahabari Jumapili.

“Iwapo serikali haitachukua hatua, tutaongoza maandamano makubwa ya wanafunzi kote Kenya. Tuko tayari kupigania haki zetu na hatutasita hadi serikali iridhie matakwa yetu,” akasema Bw Oluoch.