HabariHabari za Kitaifa

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi waandamana kupinga mfumo mpya wa ufadhili

Na TITUS OMINDE September 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Moi bewa kuu la  Kesses mjini Eldoret waliandamana Jumatatu wakitaka kufutiliwa mbali au kubadilishwa kwa mfumo mpya wa ufadhili wa masomo ya chuo kikuu.

Yalijiri licha ya viongozi wa kitaifa wa wanafunzi wa vyuo vikuu kupiga breki maandamano waliyopanga kufanya kote nchini kuanzia wiki hii, baada ya serikali kuahidi kwamba ungetathmini upya mfumo huo wa kufadhili elimu ya juu.

Hata hivyo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi walishiriki maandamano kwa kuimba nyimbo za kupinga serikali na kubeba mabango yaliyopinga mtindo huo mpya wa ufadhili. Waliwataja viongozi wao wa kitaifa kama wasaliti.

 “Kama Chuo Kikuu cha Moi tunashikilia msimamo wetu kwamba tunakataa mtindo huu wa ufadhili. Siku 30 ambazo serikali imeomba ili kutathmini upya mfumo huo ni njama ya kutufumba macho hadi mwisho wa muhula wa sasa wa masomo,” alisema Enock Kwena mmoja  wa viongozi wa wanafunzi katika chuo hicho.

Mmoja wa wanafunzi wa somo la udaktari katika Chuo Kikuu cha Moi waliandamana mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, kupinga mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya chuo kikuu mnamo Septemba 9, 2024. PICHA | JARED NYATAYA

Wanafunzi hao walishutumu serikali kwa kutojali masaibu ya wanachuo.

Walisema hawana imani kamwe na utawala wa sasa na hususan ahadi iliyotolewa na Waziri wa Elimu Julius Ogamba; ya kuundwa kwa kamati mbili zitakazotathmini mfumo huo mpya wa ufadhili, akitoa wito kwa wanafunzi kuwa watulivu.

“Ahadi zilizotolewa na serikali ni mbinu za kudumisha mfumo huu haramu ilhali tunaendelea kuteseka. Mfumo huo utaishia kuleta ubaguzi wa kielimu nchini badala ya usawa,” mwanafunzi mwingine wa chuo cha Moi alisema wakati wa maandamano hayo katika lango kuu la chuo.