Habari za Kitaifa

Suala la mrithi wa Raila lazua tumbo joto ODM


SIASA za urithi zimeanza kunoga ODM huku kinara wake Raila Odinga akitarajiwa kujiondoa chamani na kumakinikia kampeni za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Ubabe huo umeanza kushuhudiwa wakati ambapo kamati ya chama inatarajiwa kukutana Jumatano, kujadili suala la mchakato wa kumpata mrithi wa Raila.

Bw Odinga, kwa mujibu wa kanuni za AU, anatarajiwa kujiondoa kabisa ODM na siasa za nchi mwezi ujao, kisha kujaribu bahati yake kwenye wadhifa AUC ambao una umuhimu mkubwa Afrika.

Hapo Jumanne, mkutano ambao ulikuwa umeandaliwa na wenyekiti wa ODM katika kaunti zote 47, ulilazimika kuondoa ajenda ya mrithi wa Bw Odinga kwa hofu ya mgawanyiko kutokea.

Gavana wa Kakamega, Bw Fernandes Barasa, akitetea uamuzi huo, alisema ni mapema sana kujadili suala hilo ilhali kuna kamati kuu ya chama na ngazi nyingine za uongozi chamani ambazo zinaweza kulishughulikia.

“Tumeamua kuwa ‘Baba’ bado ni kiongozi wa chama na ni mapema kwa mazungumzo yoyote ya kurithi nafasi yake kuanzishwa.

Kuna asasi ambazo zinahusika na kuteua kiongozi wa chama,” akasema Bw Barasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM, Bw Philip Etale, alisema ajenda kuu ya mkutano wa Jumatano ni uchaguzi wa chama na pia Kongamano la Kitaifa ambalo litafanyika mwezi ujao.

Bw Barasa alisema kuwa wameelezwa kuwa ni wakati wa kongamano hilo ndipo mtu ambaye atachukua uongozi wa ODM ataamuliwa.

Haya yanajiri huku Mwekahazina wa ODM, Bw Timothy Bosire, naye akisema kuwa kuna viongozi wengi ambao wanaweza kuchukua nafasi ya uongozi wa chama hata kama Raila anamakinikia kampeni za AUC.

“Tuna ngazi za uongozi wa chama ambao ni dhabiti ambapo hata Raila akikosekana hakutakuwa na pengo la uongozi,” akasema Bw Bosire.

Japo kuna baadhi ya wana ODM ambao wanapendekeza kuwe na kamati ya muda ya kuongoza chama, baadhi ya wanasiasa nao wanataka kuwe na kiongozi mpya bila suala hilo kuahirishwa.

Kati ya wale ambao majina yao yametajwa kama wanaoweza kumrithi Raila ni Gavana wa Siaya James Orengo, Gladys Wanga (Homa Bay), Simba Arati (Kisii) na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ambaye pia ni katibu mkuu wa ODM.

Siasa za urithi zinapoendelea kuzua joto, Mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa ambaye ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi, alisema Bw Orengo anatosha kumrithi Raila.

“Uamuzi wetu unasalia ule ule. Huu ni mkutano wa wenyekiti wa ODM ambao haujajadili suala hilo lakini kama Kaunti ya Nairobi, tunamuunga Gavana Orengo,” akasema Bw Aladwa.

Inadaiwa kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Wycliffe Oparanya pia anamuunga mkono Bw Orengo ambaye ni mwanasheria tajika.

Baadhi ya viongozi wanawake nao wanataka Bi Wanga ambaye hivi majuzi alipokezwa wadhifa wa mwenyekiti wa ODM, apandishwe ngazi na kumrithi Raila.

Profesa Nyongó naye amewahi kushikilia chama baada ya uchaguzi mkuu wa 2013 wakati ambapo Raila alikuwa Amerika kwa kipindi kirefu.

Kuhusu Bw Orengo baadhi ya waliojitokeza kumpinga wanasema uaminifu wake kwa Raila ni wa kutiliwa shaka hasa baada ya kupinga ushirikiano kati ya ODM na serikali.

Pia anaonekana kuegemea mrengo wa Kalonzo Musyoka na anadaiwa kuwa rafiki ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, wote ambao wanaonekana kuwa mahasimu wa Raila.