Habari za Kitaifa

Abiria mataani safari za ndege zikifutwa baada ya wafanyakazi wa KAA kugoma

Na BENSON MATHEKA September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAMIA ya wasafiri wamekwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), baada ya wafanyikazi kugoma kuanzia Jumatano usiku  kulalamikia mipango tata ya serikali ya kukodisha uwanja huo kwa kampuni ya India, Adani Enterprises.

Kampuni za Safari za Ndege zimearifu wateja kwamba mgomo huo umeathiri shughuli katika uwanja huo na kwamba safari zitacheleweshwa au kufutwa.

“Kenya Airways ingetaka kuarifu kwamba kutoka na mgomo wa baadhi ya wafanyakazi katika JKIA, kumekuwa na ucheleweshaji wa safari za kuondoka na kuwasili kwa abiria,” Shirika la Ndege la Kenya, Kenya Airways lilisema kwenye taarifa Jumatano.

Kampuni ya Jambojet, inayotoa huduma za uchukuzi wa ndege ndani ya nchi, pia ilitoa taarifa kama hiyo.

Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege vya Kenya (Kawu) walisema serikali haikuonyesha nia njema katika mfululizo wa mazungumzo kuhusu mpango wa kukodisha uwanja huo.

“Serikali haijakuwa na uwazi na nia njema. Hawajatupa stakabadhi zote tulizodai. Tunachotaka ni serikali ikomeshe mpango wa  kukodisha uwanja kwa Adani,” Katibu Mkuu wa Kawu, Bw  Moss Ndiema aliambia Taifa Leo.

Serikali imesema  kwamba katika mpango huo, kampuni hiyo ya India itaboresha uwanja wa ndege, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya pili ya ndege na kituo kipya cha abiria chini ya mkataba wa miaka 30 wa kujenga- kuendesha na hatimaye kuhamisha kwa serikali.

Wafanyakazi hao walitishia kugoma wiki moja iliyopita lakini baadaye walisitisha mgomo huo baada ya kuzungumza na serikali katika mkutano uliofanyika Ikulu.

Miongoni mwa masuala muhimu waliyoibua ni pamoja na kuwepo kwa watu wasiowafahamu, wanaodaiwa kuwa wafanyikazi wa Adani ambao wamekuwa wakizunguka JKIA wakishirikiana na maafisa wakuu wa usalama wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kenya.

Watu hao wasiojulikana, walisema, walikuwa wakifanya shughuli zisizojulikana ikiwa ni pamoja na kupiga picha mitambo mbalimbali na kufanya  tathmini ya mali hatua ambazo wafanyakazi hao walishuku kuwa zinahusiana na uendelezaji wa mpango wa ukodishaji.

Ili kusitisha mgomo, wafanyakazi hao walitaka “harakati na shughuli za siri, zisizojulikana na zisizoelezeka za wafanyakazi wa Adani na  maajenti wake kusitishwa na kukomeshwa mara moja”.

Pia walitaka ufichuzi kamili wa maelezo ya pendekezo la kukodisha uwanja wa ndege kwa Adani na wakabidhiwe stakabadhi hizo ili wazichunguzwe kabla ya kitu kingine chochote kutendeka.

Stakabadhi hizi, walisema, zitawafahamisha mchango wao wa maana katika awamu ya ushirikishi wa umma wa mradi.

Wafanyikazi hao pia walitaka kusimamishwa kwa safari iliyokusudiwa ya ujumbe wa watu 16 kwenda India katika lengo la kuendeleza ukodishaji wa uwanja wa ndege kwa Adani hadi zoezi la ushiriki wa wadau na umma litakapokamilika na “Wakenya waonyeshe kukubali mradi huo”