Habari za Kitaifa

Komeni kumezea mate kiti changu, Gachagua aonya ODM

Na BARNABAS BII, BENSON MATHEKA September 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametoa changamoto kwa vyama vingine vya upinzani kujiunga na serikali Jumuishi huku akitetea nafasi yake kama  kiongozi wa  pili mkuu nchini na kuonya kuwa kuwa kiti chake hakiko wazi, na wanaokimezea mate wanapaswa kukoma.

Alivitaka vyama vingine vya upinzani kuiga chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga na kuwa sehemu ya serikali  jumuishi ili kushirikiana katika kuinua uchumi wa nchi.

“Sasa tuna ODM serikalini na vyama vingine vya upinzani viko huru kujiunga ili kuwa sehemu ya mafanikio na lawama katika chochote tunachofanya. Hata hivyo, hawafai kutarajia kuchukua nyadhifa za wengine – hasa changu kama Naibu Rais,” alisema Naibu Rais akiwa Olessos, Kaunti ya Nandi.

Naibu Rais pia alionyesha kujitolea kumuunga mkono Rais William Ruto kutimiza ahadi zake, akibainisha kuwa utawala wa Kenya Kwanza ulikuwa tayari kufanya kazi na wapinzani wake wa kisiasa chini ya mpangilio mpya wa serikali.

Aliwakemea wakosoaji wake akiwataka kuwa wanyenyekevu na kwenda polepole katika azma zao za kisiasa.

“Wale ambao wamepata rasilimali nyingi hawafai kutapika miguuni mwa wasio nazo. Wanapaswa kuwa wanyenyekevu na kutafakari historia yao,” akasema Bw Gachagua.

Alikiri kwamba shughuli katika kaunti zimelemazwa kufuatia serikali ya kitaifa kuchelewesha  kutoa pesa baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.

“Ninajua matatizo ya kifedha ambayo serikali ya kaunti imepitia kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, tungetaka zipokee angalau asilimia 50 ya pesa lakini hilo haliwezekani kwa sababu ya sheria,”  Naibu Rais alisema, akibainisha kuwa hivi karibuni Bunge itaanza tena kusaidia kupitia Mswada huo.

Kaunti  47 zinadai zaidi ya Sh90 bilioni ambazo hazijatolewa na Serikali ya Kitaifa jambo ambalo limelemaza utoaji wa huduma.