Habari za Kaunti

Kaunti ya Kericho kutumia droni kusambaza dawa hospitalini

Na VITALIS KIMUTAI September 13th, 2024 2 min read

KAUNTI ya Kericho sasa itaanza kutumia droni kuwasilisha dawa kwenye vituo vya afya 210, hatua inayolenga kusaidia kupunguza vifo wakati dharura inahitajika.

Kupitia ushirikiano na Zipline, kampuni ambayo inawasilisha droni hizo, serikali ya kaunti inalenga kuhakikisha dawa zinawasilishwa kwa wakati kwenye hospitali mbalimbali.

Aidha kutumika kwa ndege hizo zisizokuwa na rubani zitasaidia kupunguza kwa muda wa kusafirishwa kwa damu kwa wagonjwa ambao wanahitaji kuhudumiwa kidharura.

Gavana Erick Mutai alizindua kutumika kwa droni hizo katika Hospitali ya Kaunti Ndogo za Soin Sigowet mnamo Jumanne akisema kuwa matumizi ya teknolojia yatasaidia sana wakati wa dharura,

“Kutumika kwa droni katika kutoa huduma za dharura  kunaoana na mpango wetu wa kupunguza idadi ya vifo vinavyotokea hasa wakati wanawake wanapojifungua kwenye hospitali zetu,” akasema Dkt Mutai.

Droni zina uwezo wa kubeba mizigo ya  kilogramu tatu na inaweza kutumika kubeba chanjo na dawa nyingine kupelekwa maeneo mbalimbali ya kaunti.

Droni pia ina vifaa vya kiteknolojia ambavyo huvisaidia kukwepa ndege, miti, mijengo na kuna usalama mkubwa katika matumizi yake kuwasilisha mizigo.

Kericho, ndege hizo zisizokuwa na rubani zitatumika kuwasilisha dawa kwa wale ambao wameumwa na nyoka katika maeneo ambayo wanyama hao hatari huwatatiza wakazi.

Gavana Mutai alisema matumizi ya teknolojia hiyo ndiyo itamsaidia kufanikisha mpango wake wa kuboresha sekta ya afya.

“Kwa sasa wagonjwa watakuwa wakihitajika kutangamana na madaktari hata bila kufika hospitalini. Wananchi watahisi thamani ya ugatuzi kwa kuwa huduma za afya zitakuwa zikiwafikia kwa wakati,” akasema Bw Mutai.

Meneja wa Kampuni za Zipline Sineka Samuel Siabnaa  alishukuru kwa ushirikiano kati yao na kaunti. Alisema kuwa matumizi ya teknolojia ambayo yamekuwa yakienezwa na kampuni yamefanikishwa katika nchi nyingine,

Matumizi ya teknolojia hiyo yamesaidia  katika kupunguza idadi ya watoto wanaoaga dunia wakati wa kuzaliwa kwa asilimia 15 nchini Ghana na kuimarisha huduma za afya Rwanda.

“Lengo letu ni kuwafikia wagonjwa ambao wana mahitaji katika maeneo ya mashinani. Katika Kaunti ya Kericho tunaweza kuwasilisha dawa kwa dakika 55 katika eneo ambalo ni mbali sana kutoka kituo chetu,” akasema Bw Siabnaa.