Makala

Simanzi mtoto akipasua mbarika kuwa baba yake amefariki Kisumu

Na KNA September 14th, 2024 2 min read

KIINI cha mwanaume mwenye umri wa miaka 39 kujiua akiwa nyumbani mwake Manyatta viungani mwa jiji la Kisumu kingali kitendawili kwa jamaa na majirani.

Kinachojulikana kufikia sasa ni kuwa Washington Obat aligombana na mkewe Caroline Achieng mara kadhaa Alhamisi kabla ya tukio hili la kutatanisha kusababisha wingu la simanzi kutanda eneo la Manyatta.

Mke wa marehemu anasimulia kuwa walikuwa na mzozo Alhamisi jioni.

Baada ya mzozo, mume wake alimwomba msamaha warudieni na kuendeleza familia.

Ilikuwaje baadaye Obat ‘alijitia kitanzi’?

Mzozo mkali

Mkazi huyu wa Wadi ya Kondele anafichua kuwa walikabiliana vikali na mumewe katika patashika iliyomsabibishia majeraha mwilini.

Kulingana na Achieng’, isingalikuwa shangazi za mume wake, pia yeye angekuwa marehemu kama mume wake.

“Kwa bahati nzuri niliokolewa na shangazi zake na ilibidi nilale kwa majirani kuepuka hatari zaidi,” alisimulia.

“Alikuja kwa familia yangu na kunishawishi kwamba turudi nyumbani na tukapatana. Baadaye aliondoka kuelekea kazini lakini alirudi akiwa mlevi na kuanza kunisumbua huku akiniuliza nina tatizo gani. Hapo ndipo alifunga mlango na kuanza kunipiga. Nilijaribu kutoroka na kuripoti katika kituo cha polisi cha Manyatta.”

Achieng anaeleza kwamba alimtuma mwanawe nyumbani kwao kuchukua sare za shule.

Kwa bahati mbaya, anasema, mtoto wake alikutana na mwili wa baba ukilala bila pumzi.

“Nilikuwa nimemtuma mwanangu aende kuchukua sare yake kutoka nyumbani Ijumaa asubuhi lakini alimkuta baba yake tayari amekufa,” alisema.

Chifu Msaidizi wa Kata ndogo yaa Manyatta A, Agnes Akinyi alithibitisha kisa hicho na kufichua kuwa ripoti hiyo ilitumwa kituoni na mzee wa kijiji cha eneo hilo Isaac Opiyo.

“Tulipokea ripoti kutoka kwa mzee wa kijiji chetu Opiyo, kwamba mwanamume anayejulikana kama Washington Obat amejiua kufuatia ugomvi wa kifamilia,” Akinyi alifichua.

Chifu huyo msaidizi alitoa wito kwa wanandoa kutafuta usaidizi kutoka kwa afisi za serikali na mashirika mengine ya eneo hilo wakati wowote ndoa zao zinaingia doa.

Aliwaonya wanandoa dhidi ya kujichukulia sharia mkononi.

“Ikiwa wanandoa wanatofautiana basi ni bora kutafuta suluhu ya amani badala ya kujitoa uhai kwa sababu hiyo si suluhu,” alitanguliza. “Ombi langu kwa wanandoa ni kuwa karibu na afisi za serikali ili kusaidia kutatua masuala yao,”

Kadhalika, Bi Akinyi aliwahimiza wakaazi kutambua dalili za mizozo inayoweza kuwaletea balaa baadaye.

Wanapotambua changamoto za awali, aliendelea, wanafaa kushirikiana na kuhusisha uongozi wa mtaa kuwasaidia.