Jamvi La SiasaMakala

Mzigo wa kuvunja mgongo alioachiwa Nyong’o ODM

Na CHARLES WASONGA September 14th, 2024 2 min read

CHAGUZI za mashinani na mageuzi ya katiba ya ODM ndio shughuli mbili muhimu ambazo kaimu kiongozi wa ODM Peter Anyang’ Nyong’o anatarajiwa kukabiliana nazo kabla ya mwaka ujao.

Kazi ya kuongozwa shughuli hizi inamsubiri Gavana huyu wa Kisumu kando na kuongoza mikutano ya Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) ya chama hicho hadi wakati huo, wajibu ambao umekuwa ukitekelezwa na Raila Odinga aliyejiondoa kwa muda Jumatano.

Profesa Nyong’o alitwikwa wajibu wa kuongoza ODM katika kauli ya pamoja iliyofikiwa kwenye mkutano wa CMC ambako kulitangazwa kuwa uchaguzi wa ODM utaanza November mwaka huu.

Ni baada ya shughuli hiyo ambapo Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) litafanyika kuidhinisha au kukataa maafisa wa kitaifa walioteuliwa mwezi jana kushikilia nyadhifa husika kwa muda.

Wao ni pamoja na; kaimu Mwenyekiti wa Kitaifa Gladys Wanga na kaimu manaibu kiongozi; Abdullswamad Sheriff Nassir, Simba Arati na Godffrey Osotsi. Maafisa hao walijaza nafasi za John Mbadi (mwenyekiti wa zamani) pamoja na Mbw Wycliffe Oparanya na Ali Hassan Joho (manaibu kiongozi) waliong’atuka baada ya kuteuliwa kuwa mawaziri serikalini.

Kulingana na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna Kamati ya Kitaifa Shirikishi kuhusu Chaguzi (NECC) tayari imeagizwa kuanza maandalizi ya uchaguzi wa mashinani.

“Ni baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa mashinani utakaoanza Novemba mwaka huu ambapo ODM itaandaa kongamano la kitaifa la wajumbe kujaza rasmi nyadhifa kadhaa katika afisi ya kitaifa,” Seneta huyo wa Nairobi akawaambia wanahabari baada ya mkutano huo ulioongozwa na Bw Odinga, kabla ya kumpisha Profesa Nyong’o.

Bw Odinga ameamua kuzamia zaidi kampeni zake za uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Duru katika ODM zimeiambia safu hii kwamba ni katika mkutano wa NDC ambapo marekebisho kadhaa kwenye Katiba ya chama hicho yataidhinishwa na wajumbe wa chama hicho kutoka pembe zote za nchi.

“Kwa mfano, wajumbe watahitajika kuidhinisha uwepo wa nafasi tatu za manaibu wa kiongozi wa chama. Hii ni kufuatia uteuzi wa Bw Osotsi, Arati na Nassir kwa wadhifa huo,” akasema afisa mmoja anayehudumu katika makao makuu ya ODM.

Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma amethibitisha kuwa mapendekezo kadhaa yamewasilishwa yakilenga kuifanyia mageuzi katiba ya ODM na ambayo sharti yaidhinishwe katika mkutano wa NDC.

“Kwa mfano, kando na kuhalalishwa kwa nyadhifa tatu za manaibu kiongozi wa chama, majukumu ya kila mmoja wao pia yatapenyezwa katika katiba yetu. Aidha, kuna wale wanaopendekeza kuwa ibainishwe nani kati ya watu hao ndiye mwenye mamlaka ya juu kuliko wenzake. Haya yote yatashughulikiwa katika kongamano la NDC,” anaeleza.

Kulingana na mbunge huyo anayehudumu muhula wa tatu, suala hilo pamoja na uchaguzi wa mashinani ndio baadhi ya mambo ambaya Profesa Nyong’o kama kaimu kiongozi atayashughulikia kuanzia sasa.

Lakini kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Tom Mboya uchaguzi wa mashinani wa ODM ndio utakuwa mtihani mkubwa kwa Profesa Nyong’o kama kaimu kiongozi wa ODM.

“Japo Profesa Nyong’o anayo mzoefu mkubwa katika usimamizi wa masuala ya chama hicho kwa misingi kuwa amewahi kuhudumu kama Katibu Mkuu kwa muda mrefu, bila shaka atakoseshwa usingizi na joto la uchaguzi wa mashinani katika ODM. Mambo yakienda mrama, yeye ndiye ataelekezewa lawama,” anaeleza.

Kulingana naye, itamlazimu Gavana huyo wa Kisumu kukumbatia hekima ya Suleimani kukabiliana na fujo zinazoibuka nyakati za chaguzi za ODM.

“Suala hilo huwa ni nzito zaidi kiasi kwamba nyakati fulani limeonekana kumlemea Bw Odinga; ilivyoshuhudiwa mnamo 2014 ambapo uchaguzi wa kitaifa usambaratishwa na fujo katika uwanja wa Kasarani, Nairobi,” anaeleza Profesa Mboya.