Kalonzo: Ruto hajafanya kazi, ni ahadi hewa tu anazotoa
KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka, amesema kuwa utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza uko chini ya wastani kwani inatoa ahadi hewa na kuvunja sheria.
Maoni ya Bw Musyoka yanajiri huku serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto ikimaliza miaka miwili uongozini.
Bw Musyoka ambaye mnamo Jumamosi, Septemba 14, 2024 alikutana na wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka eneo la Mlima Kenya alikashifu visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara vinavyotokea kote nchini akisema kuwa Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi Gilbert Masengeli anafaa kuwajibika.
“Kwa miezi michache iliyopita, vijana wa Gen Z wamethibitisha kuwa nchi hii ni yao. Tunahitaji utawala bora, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria. Utekaji nyara bado unaendelea na Kaimu Inspekta Jenerali hajawajibika,” alisema Bw Musyoka.
Kando na hayo, alitilia maanani siasa za eneo la Mlima Kenya akisema kuwa majaribio ya hivi majuzi ya baadhi ya wabunge wa Kenya Kwanza kujitenga na Naibu Rais Rigathi Gachagua ni mpango wa Rais William Ruto wa kugawanya nchi.
“Walikuwa wakisema kwamba watajiunga na serikali lakini sasa kuna serikali ya nusu mkate. Unakosea sana kwa kujaribu kugawanya eneo la Mlima katika Magharibi na Mashariki ili upate umaarufu kisiasa. Wenye mlima watasimama imara. Vijana wa Gen Z wako imara na macho na hawataruhusu hilo kutendeka,” aliongeza.
Kiongozi huyo wa Wiper aidha alikashifu mpango wa serikali ya Kaunti ya Nairobi wa kutaka kuhamisha wafanyabiashara hadi katika soko la Kang’undo.
Aliwataka wafanyabiashara hao wakatae kuhamishwa.
“Hii ni serikali ya ahadi hewa. Huwezi kuahidi kuwainua wafanyabiashara kisha ukaendelea na kuwahimiza wahamie sehemu nyingine. Hawa ni Wakenya wanaolisha familia yao jijini Nairobi. Ukishahamisha watu kutoka hapa wataenda wapi?” Bw Musyoka alihoji.
Mbali na hayo, Bw Musyoka alitilia shaka mtindo wa ufadhili wa vyuo vikuu ulioanzishwa na serikali ya Kenya Kwanza na kusisitiza kuwa wahadhiri na wanafunzi hawauelewi.
“Hakuna anayeelewa mfumo huo wa ufadhili. Wanafunzi hawaelewi. Kando na hayo wahadhiri hawaielewi na serikali ya Kenya Kwanza pia ni kama haielewi mfumo huo. Hakuna mashauriano yanayofaa kufanywa na msikubali. Hata mimi nilishawahi kuwa waziri wa elimu na nawashauri kuwa mfumo huo wa ufadhili haufai,” akaongeza Bw Musyoka.
Alikuwa ameandamana na viongozi wengi wa kisiasa akiwemo aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na Wakili Ndegwa Njiru, miongoni mwa wengine.