Tiketi za SGR: DPP sasa aitisha faili za Wachina
Na PHILIP MUYANGA
MKURUGENZI wa mashtaka ya umma Noordin Haji ameitisha faili ya raia watatu wa China waliokamatwa kuhusiana na uchunguzi wa kashfa ya tiketi za reli ya SGR na walioshtakiwa na shtaka la kutoa jumla ya Sh900,000 kama hongo kwa maafisa wa polisi, mahakama imeambiwa.
Kiongozi wa mashtaka Bi Wangari Mwaura aliiambia mahakama ya kuwa DPP alikuwa ameomba faili hiyo kwa minajili ya kutoa maagizo.
“Kesi hii inaweza kutajwa kwa muda wa mwezi mmoja kutoka sasa ili upande wetu wa mashtaka uweze kupokea maagizo kutoka kwa DPP,” alisema Bi Mwaura hapo Jumatatu wakati wa kutajwa kwa kesi.
Bi Mwaura pia aliiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka ulikuwa na stakabadhi (ambazo wananuia kutumia katika kesi hiyo) ambazo ziko tayari kupeanwa kwa mawakili wa utetezi.
Bw Li Gen, Li Xiaowu na Sun Xin walikamatwa kuhusiana na uchunguzi wa kashfa ya tiketi za reli za SGR.Watatu hao ni meneja wa uchukuzi,afisa wa usalama na mfasiri.
Kupitia wakili wao,washtakiwa hao watatu waliiambia mahakama ya kuwa wako na hamu ya kutaka kesi dhidi yao kuanza kusikizwa.
Waliiambia mahakama kuwa wanahitaji kupewa stakabadhi zilizobakia na upande wa mashtaka ili waweze kujitayarisha kusikiza kesi.
Hakimu mkuu wa Mombasa Julius Nang’ea alipatia upande wa mashtaka wiki mbili kupata maagizo ya mkurugezi wa mashtaka na kuwapatia upande wa utetezi stakabadhi zilizobaki.
Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya Sh500,000 sawa na mdhamini wa kiasi hicho ambaye ni raia wa Kenya.
Alipowaachilia kwa dhamana,hakimu aliwaamuru washtakiwa hao kuweka passpoti zao mahakamani na aliwaonya dhidi ya kuingilia uchunguzi wa kesi la sivyo dhamana yao ifutiliwe mbali.
“Washtakiwa wanaonywa ya kuwa jaribio lolote la kuingilia (uchunguzi) litafuatwa na kufutiliwa mbali kwa dhamana,” alisema Bw Nang’ea katika uamuzi wake.
Washtakiwa walishtakiwa kwa pamoja na shtaka la kupeana Sh500,000 kama hongo kwa inspekta Andrew Warui na kundi lake la wachunguzi kama kishawishi katika uchunguzi.
Walikabiliwa na shtaka lingine la kupeana Sh200,000 kama hongo.Bw Xiaowu alikabiliwa na shtaka lingine la kupeana Sh200,000 kama hongo.
Kesi itatajwa Februari mosi.