Mpango wa Kaunti ya Nairobi kukabili saratani
HUKU takwimu zikiashiria ongezeka la visa vipya vya saratani duniani, Kaunti ya Nairobi imezindua mpango utakaowezesha kubuni mikakati mahsusi ya kukabiliana na gonjwa hilo katika jiji kuu.
Kupitia ripoti mpya kuhusu hali ilivyo jijini, Kaunti ya Nairobi imetambulisha changamoto kuu zinazozuia wagonjwa wa saratani kupata huduma bora za matibabu ikiwemo bima isiyotosheleza mahitaji ya wagonjwa.
Ufadhili duni unaotolewa na Bima ya Kitaifa kuhusu Afya Nchini (NHIF) iliyovunjiliwa mbali na Bima ya Afya ya Kimsingi (PHI) ni miongoni mwa vikwazo vinavyotatiza matibabu ya saratani kwa watoto na kuongeza gharama ya matibabu kwa wagonjwa na wanajamii jijini.
Utafiti huu ulifanywa na Kaunti ya Nairobi kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Wakfu wa Cancer Challenge (C/CAN) na unapendekeza kuwa mpango wa ufadhili kupitia bima unapaswa kuambatana na mwongozo wa matibabu.
“Ainisha saratani kulingana na mkondo wa matibabu ili kubaini viwango vya ufadhili,” inasema ripoti hiyo.
Kiasi kikubwa cha pesa wanazolazimika kutoa wanajamii ili kugharamia matibabu ya saratani yakiwemo matatizo ya kuwatuma wagonjwa kupata matibabu katika taasisi za umma na za kibinafsi ni miongoni mwa masuala yanayolemaza juhudi za kukabiliana na saratani Nairobi.
Nairobi ilijiunga na Mtandao wa Majiji dhidi ya Saratani Duniani 2022 na kuwa mji nambari 11 duniani na moja kati ya miji minne barani Afrika ikiwemo Abuja, Kigali and Kumasi.
“C/Can imetuwezesha kupata data na kufanya utafiti halisi unaotupa maelezo kuhusu kinachohitajika kwa kuturuhusu kuelewa mazingira yetu kuhusu jiji,” alisema Waziri wa Afya katika Kaunti ya Nairobi, Suzanne Silantoi.
“Mara nyingi ungepata maelezo yanayohusu taifa lote kwa jumla bila kuangazia Nairobi binafsi lakini jiji kuu lina mahitaji ya kipekee mno ambayo ni tofauti ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.”
Kando na kuwa jiji kuu, Nairobi ni moja kati ya miji mitano nchini na ni moja kati ya kaunti tatu zenye idadi kubwa zaidi ya visa vya saratani ikiwemo Kiambu na Nakuru.
Takwimu zinaashiria kuwa visa vipya vya saratani vimekadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 120 katika miongo miwili ijayo huku zaidi ya nusu ya visa vyote (asilimia 70) vikiwa katika mataifa maskini ikiwemo Kenya.
Kufikia sasa, zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani wanaishi mijini huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka hadi asilimia 66 kufikia 2050.
“Huku kiwango kikubwa cha ukuaji mijini kikitarajiwa kufanyika katika mataifa maskini, tunaamini tupo katika nafasi bora ya kuendesha ubunifu katika huduma ya afya inayohusu saratani na kujenga mifumo imara kuanzia mashinani,” alisema Mkurugenzi wa Kiufundi C/Can, Alfredo Polo.