Habari za Kitaifa

Kalonzo: Ruto hana nia njema kuhusu uteuzi wa IEBC


KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amemtaka Rais William Ruto kuharakisha mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akisema kutokuwepo kwa makamishna hao kunawanyima Wakenya haki ya uwakilishi.

Bw Musyoka alisema ukosefu wa nia njema ya kisiasa unazuia utekelezaji wa sheria iliyoundwa Juni 2024 baada ya wabunge kupitisha Mswada wa marekebisho ya Sheria ya IEBC ya 2023.

Sheria hiyo inapendekeza kuundwa kwa jopo jipya la kuteua makamishna wa IEBC lenye wanachama tisa na hivyo kuharamisha uwepo wa jopo la zamani lenye wanachama saba liloongozwa na Kasisi Daktari Nelson Makanda.

“Inasikitisha kuwa IEBC bado haina makamishna watakaotekeleza mageuzi muhimu yanayohusiana na masuala ya uchaguzi. Hamna nia ya kisiasa. Kuingiliwa kwa asasi za umma ndiko kumezuia kuwepo kwa tume halali itakayoweza kutekeleza majumu yake ya kikatiba,” Bw Musyoka akasema.

Akaongeza: “Majukumu muhimu ya IEBC ambayo yamekwama ni kama vile kufanyika kwa chaguzi ndogo katika maeneo bunge na wadi kadhaa ambazo hazina wawakilishi, uwekaji upya wa mipaka ya maeneo wakilishi na utayarishaji wa sera mbalimbali za kufanikisha utendakazi wa tume hiyo.”

Bw Musyoka alisema hayo Jumanne wakati wa Kongamano la Kitaifa Kuhusu Kukamilishwa kwa Mageuzi mfumo wa Uchaguzi kuelekea 2027.

Kiongozi huyo wa Wiper vile vile alililaumu Jopo la Kutatua Mizozo inayohusiana na Vyama vya Kisiasa (PPDT) akisema imekosa kuzingatia kanuni ya usawa wa kijinsia katika uamuzi wake kuhusu uteuzi wa wanachama wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC.

Bw Musyoka, alikuwa amewasilisha jina la Balozi Koki Muli kuchukua nafasi moja iliyotengewa muungano wa Azimio kati ya nafasi tatu zilizotengewa Kamati ya Ushirikishi wa Vyama vya Kisiasa (PPLC) katika jopo la kuteua makamishna wa IEBB.

Lakini mnamo Jumanne wiki jana, PPDT iliamua kuwa jina la Augustus Muli wa chama cha National Labour Party (NLP) ndio liwasilishwe na Azimio kama mwakilishi wake katika jopo hilo la watu tisa.

Asasi zingine ambazo zinatarajiwa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao katika jopo hilo ni Chama cha Mawakili Nchini (LSK), Baraza la Madhehebu Nchini (IRC), Chama cha Mahasibu Nchini (ICPAK) na Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Majina hayo yote yanapasa kuwasilishwa kwa tume ya PSC kisha yawasilishwe kwa Rais Ruto kwa uteuzi rasmi.

Ni baada ya kuteuliwa rasmi kwa wanachama wa jopo hilo ambapo litaapishwa na kuweka matangazo magazetini kuwaalika Wakenya waliohitimu kuwasilisha maombi ya kutaka kujaza nafasi ya mwenyekiti wa IEBC na makamishna sita.

IEBC ilisalia bila mwenyekiti na makamishna kuanzia Januari 17, 2023 muhula wa kuhudumu wa aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu ulipokamilika.

Awali, mnamo Desemba 2022 makamishna wengine watatu Juliana Cherera (Naibu Mwenyekiti) pamoja na Francis Wanderi na Justus Nyang’aya walilazimishwa kujiuzulu.

Aidha, Irene Masit alipigwa kalamu na jopo lililoteuliwa kuchunguza uhalali kuhusu tuhuma kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyomtawaza Dkt Ruto kuwa mshindi 2022.