Kwa nini maneno ‘Kitu Kidogo, muratina, busaa, chang’aa,’ yameingizwa katika kamusi ya Kingereza?
BAADHI ya maneno ya Kiswahili yameendelea kuingizwa katika kamusi ya Kingereza ya Oxford English Dictionary.
Mafungu ya maneno ‘Kitu Kidogo’ na ‘Panya Route’ ni kati ya maneno ya hivi punde zaidi kuingizwa katika kamusi hiyo.
‘Kitu kidogo’ hutumika kueleza kuhusu pesa ambazo hutolewa kwa njia ya hongo.
Na ‘Panya Route’ ni kichochoro ama njia ya siri ambayo aghalabu hutumika katika shughuli za ulanguzi.
Shirika la uchapishaji la Oxford University Press limeeleza kuwa lugha ya Swahili ni lingua franka.
Lingua Franka ni lugha ambayo hutumiwa na watu wa lugha tofauti kwa ajili ya mawasiliano.
Kiswahili ni mfano mzuri wa lingua franka sababu hutumiwa kuunganisha watu hasaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kulingana na Oxford University Press, Swahili imechangia idadi kubwa ya maneno ya mkopo katika Kingereza cha Africa Mashariki tangu 1806.
Fungu jingine la maneno ambayo yamekuwa maarufu na kuingizwa kwenye kamusi ya Kingereza ni ‘Panya Route.’
“Mseto huu wa ukopeshaji katika lugha unaunganisha neno panya (mouse kwa Kingereza) na ‘Route’ (neno la Kingereza linalomaanisha njia ama barabaraba),” shirika hilo lilieleza.
Maneno haya mapya katika kamusi hiyo yanachanganywa na mengine ambayo Oxford ilikopa awali.
Maneno mengine ya Kiswahili na ya lugha zinazotumiwa sana Kenya ni pamoja na nyama choma, asante sana, jembe, sambaza, mpango wa kando, chapo, uhuru, githeri, chang’aa, busaa, come-we-stay, jembe, buibui, sheng, muratina, kamba, sufuria, merry-go-round, isukuti, jiko, mandazi na mabati.
Pamoja na maneno ambayo yanatumika sana katika mawasiliano Kenya, Oxford imejumuisha maneno kutoka mataifa ya Uganda, Rwanda, Burundi na Mauritius.
Shirika hili huorodhesha maneno mapya kufuatia utafiti thabiti na huru kutoka kwa vyanzo tofauti.
Mchakato huu hutilia mkazo maneno ambayo yametumika kwa muda mrefu kiasi.
“Kwa viwango vya juu sana, yaliyomo kwenye lugha za Oxford huandaliwa kwa njia maalumu na kutolewa na kikosi cha wataalamu wanaohusisha watalaamu wa kuunda kamusi, wataalamu wa isimu na wanateknolojia wa lugha,” shirika hilo lilisema.
Kamusi ya Kingereza ya Oxford inatambuliwa sehemu nyingi kuwa kitabu kinaheshimiwa sana kuhusiana na lugha ya Kingereza. Ni mwongozo maarufu unaoeleza maana, historia na matamshi ya maneno 600,000 – ya kale na sasa – katika maeneo ambapo Kingereza kinazungumzwa duniani.