NLC kulipa fidia kwa visa 1,000 vya dhuluma za kihistoria kuhusu ardhi
ANGALAU visa 1,000 vya ukiukaji wa haki kuhusu umiliki wa ardhi zinachunguzwa na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kwa nia ya kuwalipa waathiriwa fidia.
Visa hivyo vimetajwa katika mawasilisho kutoka kwa jamii ya Ogiek inayoishi katika kaunti za Bungoma, Trans Nzoia, na Elgeyo Marakwet.
Tume hiyo pia inapokea mawasilisho kutoka jamii za Sabaot, Kony, Bungomek, Sengwer, Elgon Masai na Cherang’any kutoka kaunti hizo tatu.
NLC imezihakikishia jamii hizo, zilizotendewa dhuluma hizo kabla na baada ya uhuru kwamba zitapata haki na fidia ikiwa uchunguzi unaoendelea utatoa pendekezo kama hilo.
Kwenye vikao vilivyofanyika mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, NLC ilisema nyingi za malalamishi iliyopokea yana mashiko.
Kamishna wa tume hiyo Profesa James Tuitoek alifichua kuwa kati ya malalamishi 3, 742 yaliyopokewa na tume hiyo, jumla ya 1,000 yamebainika kuwa na mashiko na kuwasilishwa katika hatua ya kuchunguzwa.
“Visa hivyo, 1,000 sasa vitachunguzwa kwa kina na uamuzi kutolewa kuhusu iwapo jamii husika zitalipwa fidia,” akasema.
Makundi mengine ambayo malalamishi yao yatashughulikiwa katika kiwango cha uchunguzi ni pamoja na wakazi karibu na msitu wa Kiboroa katika eneo la Mlima Elgon na kundi la Sina Glade kutoka Msitu wa Embobut, miongoni mwa mengine.
Profesa Tuitoek alisema kuwa vikao hivyo ni sehemu ya juhudi za NLC za kuhakikisha kwa malalamishi yote kuhusu dhuluma za kihistoria kuhusu ardhi zinasuluhishwa.