Habari za Kitaifa

Gachagua hapumui hoja ya kumsuta ikitua Seneti


MASAIBU ya kisiasa yanayomkumba Naibu Rais Rigathi Gachagua yanaendelea kushika kasi huku Seneta wa Tana River Danson Mungatana akiwasilisha hoja ya kujadili mienendo yake katika Seneti.

Wadadisi wa siasa wanasema mwelekeo ambao seneta huyo amechukua ni sehemu ya mikakati ya wanaopanga kuwasilisha hoja ya kumtimua Bw Gachagua mamlakani

Bw Mungatana aliwasilisha hoja hiyo kwa Spika wa Seneti Amason Kingi, akimsuta Bw Gachagua kwa kutoa matamshi yasiyofaa na kudhihirisha mienendo inayoshusha hadhi ya Afisa ya Naibu Rais.

Seneta huyo alisema amekasirishwa na kile ambacho alikitaja kama mwenendo wa Bw Gachagua kuangazia zaidi eneo la Mlima Kenya ilhali afisi yake iko chini ya asasi ya Urais na inapasa kuangazia na kuhudumia taifa zima.

Hata hivyo, tofauti na hoja ya kumtimua afisa afisini, hoja kama hii ya Bw Mungatana inatoa tu nafasi kwa maseneta au wabunge kujadili mienendo ya mtu fulani ambayo hawakubaliani nayo.

Maseneta hawahitajiki kupiga kura baada ya kukamilishwa kwa muda unaotengewa hoja kama hiyo.

Endapo hoja ya Bw Mungatana itaidhinishwa na Bw Kingi, maseneta wote 67 watapata fursa ya kipekee kujadili mienendo ya Bw Gachagua katika kikao cha kawaida cha Seneti.

“Leo Septemba 23, 2024, nimewasilisha hoja ya kumjadili anayeshikilia afisi ya Naibu Rais kutokana na mienendo yake ambayo haifai,” Bw Mungatana akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

“Hii ni hoja ambayo nimewasilisha katika afisi ya Spika wa Seneti. Ikiidhinisha itawekwa mbele ya maseneta na wataijadili kwa kina.” akasema.

Bw Mungatana alisema maseneta watapewa nafasi ya kukemea mienendo ya Bw Gachagua ambaye alisema anajifanya kama naibu rais wa eneo la Mlima Kenya.

“Sharti akumbushwe kuwa yeye ni Naibu Rais wa Kenya sio eneo moja. Mimi na watu wa Tana River tumechukizwa zaidi na mienendo ya Bw Gachagua,” Bw Mungatana akasema.

“Mbona anakiuka kiapo cha afisi ya Naibu Rais? Anapigania eneo moja tu. Nadhani Seneti ni mahala pa kuelezea mabaya ya Naibu Rais,” akaongeza.

Alisema kulingana na Katiba ya sasa, mtu anayeshikilia afisi ya kitaifa hawezi kushikilia wadhifa mwengine katika ngazi ya eneo au kaunti.

Kulingana na mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, hoja ya Seneta Mungata ni mojawapo ya hatua za kumhangaisha Bw Gachagua katika maandalizi ya kumtimua.

“Yatakayojadiliwa huko yataanika mengi, yanakusudiwa kuandaa hoja ya kumtimua itakayowasilishwa katika Bunge la Kitaifa na ikipitishwa, iwasilishwe seneti,” akasema Dkt Gichuki.

Inasemekana mikakati ya kuwasilisha hoja hiyo imeiva huku wabunge wa chama tawala cha UDA washirika wa Rais Ruto na ODM wakijipanga kumtimua ofisini Bw Gachagua.

Bw Mungata alimshutumu Bw Gachagua kwa kujifanya kama rais mwenza badala ya kufanyakazi kama msaidizi mkuu wa Rais William Ruto kauli ambayo Dkt Gichuki anasema inaashiria aina ya mashtaka dhidi ya naibu rais katika hoja ya kumtimua iwapo itawasilishwa bungeni.

Hoja ya Mungatana inajiri siku chache baada ya Bw Gachagua kujitokeza katika runinga wiki jana na kulalamikia kunyanyaswa na maafisa na wanasiasa wandani wa bosi wake, Dkt Ruto.

Akihojiwa katika runinga ya Citizen Ijumaa wiki jana, Bw Gachagua alisema kuna njama ya kumwondoa afisini.

Hata hivyo, alisema kuwa hoja ya kumwondoa afisini— aliyosema ni hatari kwa uthabiti wa taifa hili—inaweza tu kuidhinishwa na Rais Ruto.

Bw Gachagua aliweka wazi mivutano ya kimamlaka ambayo imezonga serikali ya Kenya Kwanza ndani ya miaka miwili tangu ilipoingia mamlaka akisema watu fulani wanaendesha njama ya kuhujumu utendakazi wake serikalini.