Habari za Kaunti

Msitawaliwe na ulafi wa kodi ilhali huduma hazipo, wachimba migodi wakemea utawala

Na KALUME KAZUNGU September 24th, 2024 2 min read

WACHIMBAJI mawe kwenye migodi ya Manda-Maweni, Kaunti ya Lamu, wameitaka Serikali ya Kaunti iweke kipaumbele shughuli za kuwatolea huduma badala ya ukusanyaji kodi.

Kulingana nao, Serikali ya Kaunti imezidi kuwatelekeza wakifumbia macho uboreshaji wa miundomsingi na mazingira yao ya kikazi kwa jumla ilhali wao hutozwa kodi kila mara.

“Kaunti imeleta afisa wake wa kukusanya kodi hapa kijijini Manda-Maweni. Anashughulika tu na ukusanyaji kodi ilhali miundomsingi haishughulikiwi,” akasema mmoja wao, Bw Justus Mwaniki.

Bi Loice Irungu, ambaye ni mvunjaji kokoto, alisema walitarajia kwamba kaunti ingewawekea hata taa ili kuwawezesha kutekeleza shughuli zao usiku na mchana.

Sehemu mojawapo ya machimbo ya mawe kijijini Manda-Maweni, Lamu. Wachimba mawe Jumapili, Septemba 22, 2024 waliifokea kaunti kwa kuwatelekeza kimiundomsingi na mazingira ya utendakazi. Picha|Kalume Kazungu

Bi Irungu anasema wanalazimika kufunga shughuli zao mapema jioni kutokana na giza kwenye machimbo.

“Vile tunalipa kodi ya kila siku tungependa sana kuona kaunti yetu ikiweka taa za mulika mwizi, hasa zile zinazotumia miale ya jua kwenye migodi yetu. Hili giza linahatarisha usalama wetu machimboni. Wakituwekea vitu kama hivyo ninaamini tutazifanya shughuli zetu usiku kucha,” akasema Bi Irungu.

Waziri wa Maliasili katika kaunti, Bi Tashrifa Bakari, alisema bado hawajapokea ripoti kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kuhusu shughuli zinazofanywa katika Manda-Maweni ili kuwawezesha kuingilia kati.

Alisema ni muhimu ripoti hiyo ya NEMA iandaliwe na ikabidhiwe Serikali ya Kaunti kabla ya kuanza kupanga namna ya kuwasaidia wafanyakazi wa machimbo hayo.

“Hatujakataa kusaidia wachimbaji mawe. Wawe na subira. Tunashirikiana na NEMA kuona jinsi shughuli za uchimbaji mawe zinazofanywa Manda-Maweni zilivyo salama kabla ya kuanza mpango kamili wa kuwasaidia,” akasema Bi Bakari.

Mawe yakiwa yamepangwa kwenye bandari au forodha ya kijiji cha Manda-Maweni, Lamu Jumapili, Septemba 22,2024. Picha|Kalume Kazungu

Kijiji cha Manda-Maweni, kilichoko kisiwa cha Manda, kinafahamika kwa biashara ya kuchimba na kuuza mawe na bidhaa nyingine za ujenzi kote Lamu. Zaidi ya wachimbaji mawe 2,000 hupatikana kijijini Manda-Maweni ambapo kuna sehemu nyingi zinazochimbwa mawe hayo.

Bw Fredrick Odhiambo, mchimbaji mawe, alisema wanatarajia kwamba kodi wanayotoa itumike vyema, ikiwemo kuwapokeza mafunzo ya jinsi watapanua shughuli zao za kuchimba mawe.

Bw Odhiambo alisema endapo wachimba mawe hao watawezeshwa kikamilifu, anaamini hata zabuni za kusambaza bidhaa za kujenga kwa miradi ya serikali Lamu wataweza kuzifaidi.

Wachimba migodi hao pia walimrai Waziri wa Madini nchini, Bw Hassan Ali Joho kutembelea eneo hilo na kuchanganua jinsi watakavyosaidiwa kupanua biashara yao.